Bado mjadala mdomoni kwa mashabiki wa Soka hususani wale Simba, Yanga na Coastal ni hatma ya wachezaji wawili tu. Yusuf Kagoma na Lameck Lawi.
Lakini Mwanaspoti limepata habari za uhakika kabisa kutoka ndani kwamba muda wowote kuanzia sasa zinaweza kutoka habari za kushtua kwa pande zote tatu na kuna ambaye anaweza kupoteza
Mwanaspoti limejiridhisha kutoka kwenye mamlaka za soka kwamba kuna mambo matatu yanakwenda kuwekwa rasmi kwa umma.Kagoma kutoka Singida Fountain Gate ameidhinishwa kuchezea Simba na Lawi atasalia Coastal Union pale Tanga badala ya kuhamia Simba.
Lakini siyo hilo tu. Ndani ya saa 48 kuanzia jana Yanga,Singida Fountain zinapaswa kukaa ili Kagoma arudishe fedha anazodaiwa kupokea Jangwani kabla hajaanguka Msimbazi.
KAGOMA MALI YA SIMBA
Kwa muda wa wiki kadhaa, kulizagaa taarifa kuwa klabu ya Simba kuingia matatani kwa kumchezesha Kagoma katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Fountaine Gate FC na hivyo watapokonywa pointi tatu.
Taarifa hizo zilitokana na malalamiko ya klabu ya Yanga ambayo yapo katika Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji Tanzania ambako kwa wakati huo yalikuwa bado hayajaamuliwa.
Taarifa hizo zilikwenda mbali zaidi hasa baada ya Simba kumchezesha mchezaji huyo na kudai kuwa wekundu hao wa Msimbazi wameonywa kutomtumia mchezaji huyo mpaka hapo shauri lake litakapoamuliwa.
Hata hivyo, taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti imezipata zimesema kuwa Kagoma amehalalishwa kuichezea Simba kutokana na ukweli wa kikanuni kuwa ndiyo klabu iliyokamilisha taratibu zote za usajili.
Chanzo chetu kimesema kuwa Simba ndiyo imeingia mkataba halali na mchezaji huyo na kuidhinishwa na timu yake ya Fountain Gate FC tofauti na Yanga ambayo ilisaini mkataba wa awali na mchezaji huyo.
Habari zinasema kuwa mkataba wa Simba na Kagoma unatambuliwa na Shirikisho la Kandanda nchini (TFF) kutokana na ukweli kuwa klabu hiyo (Simba) iliusajili wakati Yanga haikufanya hivyo kwa wakati na hata kwenye orodha waliyowasilisha jina lake halimo linasomeka Simba tu.
“Hapa hakuna suala la kusaini mara mbili(Simba, Yanga) kama inavyodaiwa. Pia taratibu za usajili kama inavyotakiwa na mfumo wa FIFA haziitambui Yanga kummiliki mchezaji huyo zaidi ya Simba na inaonyesha wazi kuwa ametokea klabu gani,"kilifafanua chanzo chetu kutoka TFF.
"Kama pingamizi lingewekwa na klabu ya Fountain Gate FC ambayo ndiyo ilikuwa inammiliki mchezaji ingekuwa sawa. Kimsingi, madai ya Yanga ni dhidi ya Kagoma binafsi na wala hayahusiani na klabu ya Simba,” kilifafanua chanzo chetu.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa Yanga inaweza kumdai Kagoma au klabu endapo makubaliano yao yalikuwa yanasema hivyo, lakini si kumzuia mchezaji kucheza na kwamba Simba imepewa leseni ya mchezaji huyo kuitumikia katika mashindano mbalimbali.
YUSUPH ALLY KAGOMA
Jina: Yusuph Ally Kagoma
Kuzaliwa: Aprili 3, 1996
Umri: Miaka 28
Nafasi: Kiungo Mkabaji
Timu: Geita Gold, Singida Fountain Gate, Simba SC
ISHU YA LAWI
Huyu ameidhinishwa kusalia kwenye klabu yake ya awali ya Coastal Union ya Tanga ambayo tayari alishaaga na mashabiki kwenye Uwanja wa Mkwakwani.
Simba ilifungua shauri dhidi ya Lawi ambaye inadai kumsajili, lakini Coastal Union iliibuka baadaye na kusema kuwa Simba ilishindwa kutimiza makubaliano ya kimkataba baina ya timu hizo mbili na mchezaji na dili hilo kufutika.
Lawi, ambaye alibakiwa na mkataba wa mwaka mmoja na Coastal Union, alishatambulishwa na Simba baada ya kudaiwa kukubaliana na Wagosi pamoja na mchezaji mwenyewe, lakini kitendo cha mabosi wa Msimbazi kuchelewesha fedha kiliwafanya Wana Mangushi kubadili mawazo.
Hata hivyo, chanzo chetu kilisema kuwa Kamati imezingatia makubaliano yaliyowekwa baina ya Coastal Union na baadaye kuvunjika na hivyo kumuidhinisha Lawi kuichezea Coastal Union.
"Kama Simba ilivyofaidika na suala la Kagoma, Coastal Union nayo imefaidika kwa njia hiyo hiyo. Simba haina mkataba na Lawi ambao umesajiliwa na TFF. Mkataba ambao unatambulika na TFF ni wa Lawi na Coastal Union na si vinginevyo na Coastal Union imepewa leseni ya kumtumia Lawi kuichezea katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara,"alisema.
Aidha, viongozi wa Simba na Coastal Union wamepewa nafasi ya kumalizana wao kwa wao nje ya chumba cha maamuzi, hakuna majibu hadi jana jioni.
Lawi amerejea nchini hivikaribuni kutoka kwenye majaribio katika klabu ya K.A.A Gent ya Ubelgiji na tayari ameanza kupiga tizi, lakini akakiri kuwa jambo moja ambalo linamtesa ni usajili wake.
“Nipo nchini, kwa sasa siwezi kuzungumza chochote kuhusiana na mambo yaliyotokea Ubelgiji, kikubwa ninachoweza kusema naendelea kujifua na Coastal Union, kuhusiana na kucheza sijajua hatma yangu hadi sasa,” alisema na kuongeza;
“Tangu nimerudi nipo pamoja na Coastal Union lakini mambo bado hayajakaa vizuri kwenye suala la Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ambapo ndio kesi ipo huko, hivyo mambo yakienda sawa nitacheza.”
Lawi akizungumzia namna mchakato wake wa usajili ulivyoenda alisema anapitia wakati mgumu sasa kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kuendeleza alipoishia msimu uliopita na hatimaye kufikia malengo.
“Siwezi nikawa sawa wakati sichezi na ligi inaendelea, hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa nje ya uwanja wakati anaona ana ,uwezo wa kucheza lakini naamini muda utafika nitacheza,” alisema.
LAMECK ELIAS LAWI
Kuzaliwa: Septemba 12, 2005
Umri: Miaka 18
Nafasi: Beki wa Kati
Timu: Coastal Union
KWANINI YANGA IMESHINDWA?
Imewasilisha malalamiko TFF kuhusiana na mchezaji huyo kufanya makubaliano na wao na kusaini mkataba, lakini inaelezwa kuwa kuchelewa kumalizana na uongozi wa Singida Fountain Gate ndio sababu ya timu hiyo kushindwa kumpata Kagoma.
"Kilichopo muda huu ni kwamba Yanga wanakesi ya madai na sio mchezaji kwasababu huyo tayari ameidhinishwa kuwa ni mchezaji wa Simba kwa vigezo vyote wao sasa wanamadai yao ya fedha walizokabidhiana,"kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Kitu kingine ambacho kinaifunga Yanga kuwa huyo si mchezaji wao ni kitendo cha wao kushindwa kuwasilisha jina la mchezaji huyo kwenye idadi ya majina ya wachezaji wao wa msimu huu na wasingeweza kufanya hivyo kwasababu hawakuwa na uthibitisho wa umiliki wa mchezaji."
Chanzo hicho kilisisitiza kuwa Kagoma ni mali ya Simba na Yanga wao watamalizana na Fountaine Gate kwa masuala yao ya madai na sio kummiliki mchezaji ambaye tayari ameingia kwenye mfumo wa waajiri wake wa sasa.
SAA 48 WAMALIZANE
Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji imetoa siku mbili ambazo ni sawa na masaa 48 kwa viongozi wa Yanga na Singida Fountain Gate kumalizama juu ya sakata linalomuhusu Yusufu Kagoma wa Simba.
Kikako cha Kamati hiyo mara ya mwisho kilifanyika Alhamisi ambapo viongozi wa Yanga ambao wanasimamia shitaka hilo waliomba muda wa siku mbili ili kulitatua tatizo hilo kabla ya kamati kutoa uamuzi.