Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

KYENGA:Nilimgomea kocha kwenda kwa mganga ili nishinde

Kyengaaaaa KYENGA:Nilimgomea kocha kwenda kwa mganga ili nishinde

Wed, 24 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kutoka Nyanda za Juu Kusini katika Mkoa wa Mbeya na mkoa mpya wa Songwe, jina la Alto Kyenga katika mchezo wa ngumi za kulipwa lina heshima na ukubwa wake kutokana na kuutendea haki mchezo huo licha ya figisu alizowahi kukutana nazo.

Lakini, huenda kwa wale mashabiki wa mchezo huo kupitia runinga wakashindwa kumtambua kabisa bondia huyo, lakini kwa Songwe na Mbeya amejiwekea utawala wake kutokana na ukubwa wa jina.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano sita pekee kabla ya kukacha mchezo huo kwa muda na kuweka nguvu kubwa katika biashara baada ya kufanyiwa kile anachoamini kwamba ni hujuma na makocha katika pambano la mwisho alilocheza Julai 15, 2023 dhidi ya Jacob Maganga wa Tanga.

Katika pambano hilo ambalo lilipigwa kwenye Uwanja wa Kinesi, Ubungo jijini Dar es Salaam, Kyenga alipoteza kwa TKO ya raundi ya tatu ambayo ameeleza alifanyiwa hujuma na jopo la makocha wake wakati huo kwa kushirikiana na waamuzi walioamua pambano lake.

Kyenga ameweka makazi na shughuli zake kibiashara katika eneo la Mpemba, Tunduma, akiwa amefanikiwa kushinda mapambano matatu yote kwa ‘Knockout’ na kupigwa kwenye mapambano mawili na moja kati ya hayo ni kwa ‘Knockout’.

Bondia huyo mzaliwa wa Njombe katika mapambano hayo amefanikiwa kuwachapa Julius Mwakalobo kwa ‘Technical Knockout’ ya raundi ya nne katika pambano la raundi nne, Ambokile Chusa akichapwa katika raundi ya pili kwa Chusa kushindwa kuendelea na pambano kutokana na kichapo alichokuwa akipokea.

Lakini baada ya Chusa, akaja kumtandika kwa ‘Technical Knockout’ ya raundi ya pili Six Bruno kabla ya kutoka sare na mmoja wa mabondia wakubwa kwenye mchezo huo, Selemani Galile katika pambano la raundi nane.

Kyenga alionja joto ya kichapo cha kwanza katika pambano la Mtwara Ubabe Ubabe 2 ambalo lilifanyika kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona baada ya kupigwa kwa pointi na Ibrahim Tamba katika pambano la raundi sita kabla ya kupigwa tena na Jacob Maganga ambalo ndilo lilikuwa pambano la mwisho kuonekana ulingoni.

Mwanaspoti limezikata kilomita 934 kutoka katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Mpemba, Tunduma na kufanya mahojiano maalumu na bondia huyo aliyefanikiwa zaidi nje ya mchezo huo kutokana biashara anazomiliki.

Kyenga anayepigana katika uzani wa Super Walter alianza mahojiano kwa kusimulia namna alivyokimbia shule kutokana ugumu wa maisha aliokutana nayo kwenye familia hali iliyomfanya aingie mtaani mwenyewe kutafuta pesa kwa malengo ya kuisaidia familia yake na ugumu wa maisha.

“Shule nimeishia kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Idamba ambayo ipo Njombe vijijini. Unajua nimezaliwa kijijini kabisa katika familia ya watoto tisa wa mzee Kyenga,” anasema bondia huyo na kuongeza:

“Unajua nilichukua uamuzi wa kuachana na shule mwaka 2013 ilivyofika mwezi wa nne. Nikaondoka nyumbani na kwenda mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa ajili ya kufanya kazi ya vibarua vya kulima.

“Lakini wakati nafanya kazi ya kibarua wa kulima katika mashamba ya watu bosi wangu alikuwa na moyo mzuri akanihamishia mashine ya kusaga mahindi nikawa nafanya kazi huko.”

SWALI: Kitu gani kilikufanya ufike Tunduma?

JIBU: “Unajua hapa mimi siyo kwetu kwa maana ya kuzaliwa ila nilifika hapa kwa sababu nilipokuwa nafanya kibarua cha kulima na kusaga mahindi, nilifanya kwa muda mchache sana kisha niliamua kuondoka mwenyewe kuja Tunduma.”

SWALI: Nani alikuwa mwenyeji wako Tunduma wakati huo?

JIBU: “Hapa nilikuja kwa baba mdogo kwa sababu biashara yake ilikuwa kukata mabalo ya nguo za mtumba kisha tunauza, nilikuja kwa lengo la nipate kazi ambayo nilipata.

“Nilifanya kazi ya kuuza mtumba katikati ya mpaka wa Tanzania na Zambia, nilifanya kazi ya kuuza mtumba kwa kipindi cha miaka miwili lakini baadaye nikageukia udalali wa mabalo ya mtumba kwa kuwauzia Wazambia.

“Lakini baadaye niliachana na biashara hiyo na kuweka nguvu katika biashara ya vipodozi ambavyo nilikuwa nikiuza jumla kabla ya kuachana nayo na kuingia katika biashara hii ya pombe kali na vinywaji laini kwa bei ya jumla.”

Wakati mazungumzo ya mahojiano yanaendelea katika duka lake, Alto muda mwingi alikuwa bize kufuatilia mauzo na hesabu za madeni ya watu wanaodaiwa, jambo ambalo lilifanya Mwanaspoti itake kujua amewezaje kusimamia mfumo wa ugavi kwa njia ya kompyuta ikiwa elimu yake ipo chini.

Kyenga anasema zamani alikuwa akifanya biashara kwa hesabu zote kuingizwa katika madaftari ambayo wakati mwingine yalisababisha kumpa hasara kwa kuwa mfumo wa kuandika kwenye madaftari ni rahisi kupoteza hesabu.

“Ni kweli elimu yangu ni ndogo na mfumo wangu wa hesabu ulikuwa wa kuandika kwenye daftari ambao mara nyingi ulikuwa unaleta hasara kwenye majumuisho ya mahesabu,” anasema.

“Lakini kuna rafiki yangu ni mfanyabishara mkubwa ndiye alinielekeza na kunifundisha mfumo huu wa kutunza taarifa kupitia kompyuta na umekuwa ukinisaidia mambo kwenda sawa maana biashara inataka umakini kwenye taarifa za mahesabu.

“Kiukweli unanisaidia kwenye mambo mengi, ulinzi maana oda za kuandikia mkono zinachanganya. Imefika miaka minne tangu niweke mfumo huu ilinichukua miezi miwili kujua kila kitu na jinsi ya kuendesha.”

SWALI: Ofisi yako ina wafanyakazi wangapi?

JIBU: “Hapa kuna watu saba ambao wanafanya kazi chini yangu. Wapo wa kuhakiki oda, kusambaza na kuuza na hawa wote nawalipa posho kwa siku Sh5,000 hakuna mshahara wa mkataba kwa sababu ya kuondoa usumbufu.

“Lakini mbali ya hapa Mpemba nina miradi ya biashara ya miti mbao na ipo ambayo nimelima kwenye shamba langu ekari 20, pia kuna eneo linaitwa Umalila hapo nina mashine za kuchana mbao ambazo wakati mwingine nanunua miti kwa ajili ya kuchana na kuuza.

SWALI: Vipi upande wa familia?

JIBU: “Nimeoa kwa maana naishi na mke, lakini nimejaliwa kupata watoto wa kiume wawili ambao mmoja anasoma na mwingine bado mdogo sana.

SWALI: Nini kilikufanya uingie kwenye ngumi?

JIBU: “Unajua zamani hapa Tunduma nilikuwa red brigade wa Chadema na kule tulikuwa tunafanya mazoezi ya vyuma hapo ndiyo nikaanza mchezo huu,” anasema.

“Nikawa napigana mapambano yetu madogo huku Tunduma na Mbeya lakini baada ya kuwa mfanyabiashara niliachana na mambo ya siasa ila ngumi nikaendelea nazo hadi kuwekwa kwenye mfumo rasmi.

SWALI: Ubondia na ujasiriamali upi unalipa?

JIBU: “Binafsi ujasiriamali kwangu unalipa sana kwa sababu kila siku biashara zinafanyika ingawa ubondia unaweza kukulipa ikiwa pale umekuwa na jina kubwa kwenye mchezo kama Selemani Kidunda, Twaha Kiduku au Dullah Mbabe.

“Unajua huwezi kupata pesa nyingi ikiwa rekodi (zako) ndogo kwa sababu pesa nyingi ipo kwenye rekodi katika mchezo wa ngumi.

SWALI: Nini kimekufanya usionekane kwenye ulingo kwa muda sasa?

JIBU: “Niliamua kukaa pembeni kwa muda kwa ajili ya kusimamia biashara, lakini kama unakumbuka katika pambano langu la mwisho nilipigwa, ila ni kipigo ambacho kilitokana na hujuma za kocha wangu akishirikiana na waamuzi wa pambano ambalo nilicheza.

“Binafsi sijajua kwa nini aliamua kufanya hivyo ila uamuzi niliochukua ni kujiweka pembeni kwa muda na kuweka nguvu kwenye biashara halafu nitarejea kwa sababu ngumi kwangu ni sehemu ya furaha, ila siyo sehemu ya kupata pesa.

“Lakini nachoshukuru (ngumi) zimefanya Watanzania wengi wanijue au tujuane na hilo ndilo kubwa. Kwa sasa upande wangu ambalo naliona ila faida ya pesa bado sijaona.

SWALI: Ulishawahi kwenda kwa mganga ili ushinde pambano?

“Nikwambie tu, siamini katika mambo ushirikina, lakini nakumbuka kocha niliyekuwa naye hapo nyuma aliwahi kuniambia anipeleke kwa mganga ili nishinde pambano, lakini nilimpinga.

“Nilijiuliza maswali mengi ambayo sikupata majibu kwa nini anipeleke kwa mganga ndiyo nishinde pambano, lakini msimamo wangu ulikuwa tofauti na mtazamo wake kwa sababu ushindi unapatikana kwa mazoezi,” anasema Kyenga.

Chanzo: Mwanaspoti