Simba imefikia uamuzi wa kushusha straika dakika za jioni kabla ya dirisha la usajili halijafungwa Agosti 15, mwaka huu ikiwa zimebaki takribani siku mbili pekee kutoka leo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids kutazama mwenendo wa timu hiyo katika michezo mitatu mfululizo ya hivi karibuni kuanzia Simba Day hadi Ngao ya Jamii, akiwataka mabosi wa kikosi hicho kuanza mara moja kutafuta mshambuliaji mpya atakayeongeza nguvu kikosini hapo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza mmoja wa washambuliaji waliofikia pazuri na Simba ni pamoja na Mrundi, Elvis Kamsoba ambaye kwa sasa ni mchezaji huru, baada ya kuachana na Perserikatan Sepakbola Sleman ya Indonesia.
Mwingine ni Christian Leonel Ateba Mbida raia wa Cameroon mwenye umri wa miaka 25. Katika michezo mitatu iliyocheza Simba hivi karibuni ilianza na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya APR ya Rwanda katika Simba Day, ikachapwa 1-0 na Yanga kwenye nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Baada ya hapo ikaifunga Coastal Union 1-0 katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu ndani ya Ngao ya Jamii, hivyo kocha huyo hajaridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na washambuliaji wa timu hiyo ambao ni Freddy Michael Koublan, Valentino Mashaka, Steven Mukwala na Kibu Denis waliotoka bila ya bao katika mechi hizo tatu.
Fadlu aliyetangazwa kuinoa Simba Julai 5, mwaka huu akichukua nafasi ya Mualgeria, Abdelhak Benchikha, ameweka wazi kutoridhishwa na safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, hivyo kuwataka mabosi wa kikosi hicho kuanza mchakato huo haraka.
Kamsoba mwenye miaka 28, huku akichezea timu mbalimbali zikiwemo Melbourne Victory FC na Sydney FC za Australia, ikiwa atajiunga na klabu hiyo itabidi ipunguze mchezaji mmoja wa kigeni ili kuendana na idadi ya wachezaji 12 wanaohitajika kikanuni.
Kwa upande wa Christian Leonel Ateba Mbida, hivi sasa ni mali ya USM Alger ya Algeria aliyojiunga nayo Januari 2024 akiwa na mkataba hadi Juni 2026.
Nyota waliokuwa katika mtego wa kuondolewa ndani ya Simba ni mshambuliaji raia wa Ivory Coast, Freddy Michael Kouablan aliyejiunga na Simba Januari mwaka huu akitokea Klabu ya Green Eagles ya Zambia na kufunga mabao sita ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita.
Mwingine ni kipa Ayoub Lakred aliyetua nchini msimu uliopita akitokea FAR Rabat ya kwao Morocco, licha ya kuongeza mkataba mpya na kikosi hicho wa mwaka mmoja lakini anaweza kuachwa baada ya ujio wa kipa raia Guinea, Moussa Camara aliyetoka Horoya AC ya Guinea.
Ukiachana na wawili hao, mwingine anayeweza kuachwa ili kupisha usajili wa mshambuliaji mpya ni kiungo Mkongomani, Fabrice Ngoma aliyetua Simba msimu uliopita akitokea Al Hilal ya Sudan ambaye inaelezwa yupo tayari kuondoka ndani ya timu hiyo huku akiwa na ofa kutoka Libya.
Taarifa kutoka ndani ya Simba, zinabainisha kwamba Fadlu amewataka viongozi kuhakikisha wanapata mshambuliaji mpya atakayeongeza makali ya timu hiyo msimu huu katika michuano mbalimbali ikiwemo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
“Ni kweli kocha amependekeza kuongezwa kwa mshambuliaji mwingine na taratibu hizo tayari zimeanza, ni matumaini yetu hadi wiki hii kumalizika tutakuwa tumempata japo wapo ambao tumeshaanza nao mazungumzo ya awali,” kilisema chanzo hicho.
Imani Kajula ambaye mwishoni mwa mwezi huu ataondoka rasmi Simba baada ya kumaliza muda wake katika nafasi Ofisa Mtendaji Mkuu klabuni hapo, alisema wao wana utaratibu mzuri wa kutoa taarifa zilizokuwa sahihi kwa timu hiyo, hivyo mashabiki waendelee kufuatilia mitandao yao ya kijamii na sio vinginevyo.
Msako huo wa mshambuliaji mpya unajiri baada ya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Kocha, Fadlu Davids kutoridhishwa na uwezo wa Mganda, Steven Dese Mukwala aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu, akitokea Klabu ya Asante Kotoko ya Ghana.
Nyota huyo ametua Simba huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko ya Ghana nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga mabao 16.
Pia aliibuka mchezaji bora wa Ligi ya Ghana Desemba mwaka jana akiwa na kikosi hicho cha Asante Kotoko alichojiunga nacho Agosti 2022 akitokea Klabu ya URA ya kwao Uganda na katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kutoa asisti tano.
Licha ya takwimu nzuri kwa nyota huyo ambaye aliaminiwa kuwa suluhuisho la mabao Simba, lakini bado hajaonyesha uwezo mkubwa wa kuwaridhisha mashabiki wa kikosi hicho, huku akianza vibaya maisha yake baada ya kukosa penalti dhidi ya APR ya Rwanda katika mechi ya kirafiki kwenye Tamasha la Simba Day lililofanyika Agosti 3, mwaka huu.
ISHU YA NGOMA IPO HIVI Taarifa ambazo zimefika katika dawati la Mwanaspoti zinabainisha kwamba Fabrice Ngoma anayecheza nafasi ya kiungo mkabaji ndani ya Simba, maisha yake yanaweza yasiwe marefu klabuni hapo baada ya kuwepo kwa ofa kutoka timu mbalimbali zikimuhitaji.
Ngoma kwa sasa nafasi yake inaonekana finyu ndani ya Simba chini ya Kocha Fadlu Davids, anayeamini zaidi katika vijana, kiungo huyo anashindania namba dhidi ya Augustine Okejepha, Debora Fernandes, Mzamiru Yassin na Yusuf Kagoma, jambo linalooneka linamtoa mchezoni.
Mwanaspoti limepata taarifa za ndani kwamba wakala wa mchezaji huyo, Faustine Mukandila yupo hapa nchini na juzi Jumapili alikuwepo Uwanja wa Benjamin Mkapa, kushuhudia mechi za Ngao ya Jamii, imeelezwa ana mpango wa kuzungumza na Simba kuhusiana na suala hilo.
“Kuna timu ya Saudia na Qatar ambazo zimepeleka pesa ndefu, ilionekana kushindikana viongozi wakiamini bado ana umuhimu wa uwepo wake kikosini, wakiamini ni kiongozi mzuri dhidi ya wengine na ndiye mwenye CV kubwa dhidi ya wenzake,” kilisema chanzo.
Kabla ya hapo, iliwahi kuelezwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi aliwahi kuvutiwa na huduma ya Ngoma, ingawa hakufanikiwa kuinasa saini ya kiungo huyo ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja ndani ya Simba.