Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Huu ni muda wa kupimana afya

Chadrack Boka.jpeg Huu ni muda wa kupimana afya

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wiki mbili zilizopita barani Ulaya Euro 2024 ilimalizika na bingwa ilikuwa Hispania wakati Copa Amerika 2024 ilikwisha na bingwa ni timu ya taifa ya Argentina.

Mara baada ya hekaheka hizo zilizokuwa na upinzani mkali kumalizika hivi sasa ni kipindi cha kuwageukia wachezaji wanaohama kutoka klabu moja kwenda nyingine. Wengi wao ni wale ambao katika mashindano hayo makubwa duniani walifanya vizuri mfano mojawapo ni mchezaji bora wa Copa Amerika 2024, James Rodriguez.

Wakati hapa nyumbani kama mnavyoona hivi sasa ni wakati wa kujaribu wachezaji wapya ambao tumewaona katika mechi za maandalizi na pia wanatarajiwa kucheza katika Simba Day, Wiki ya Wananchi na matamasha mengine ya klabu nchini.

Wachezaji wapya wanaonunuliwa na klabu huwa hawanunuliwi kama jezi, bali kuna mchakato mrefu ambao ndio unaofanya uwaone wakianza kutumika katika mechi za majaribio.

Wachezaji wote wapya unaowaona katika mechi hizo fahamu kuwa mchakato mzima wa kupima afya ulipita salama ndiyo maana alisajiliwa na klabu. Ligi nyingi duniani ikiwamo ya hapa nyumbani na ile Ligi Kuu Engaland (EPL) zinatarajiwa kuanza mwezi ujao. Hii ndio sababu muda huu klabu zipo katika programu maalumu ya kupimana afya.

Ndani ya Yanga tumemuona aliyekuwa kiungo wa Simba, Clatous Chama ambaye sasa ataitumikia Yanga katika msimu mpya wa 2024/25. Hii ina maana mchezaji kama Chama tayari amepita katika vipimo.

Lakini kipindi hicho siyo wachezaji wanaonunuliwa pekee ndiyo wanapima afya, bali hata wale ambao wapo klabuni muda huu na wao wanapimwa afya ili kutathimini utimamu wao wa kimwili.

UCHUNGUZI WA AFYA Katika kiwango cha wadau wa soka wasomi, mpira wa miguu hauhitaji ujuzi tu, bali ni mchanganyiko wa kipekee wa sifa za kimwili. Wachezaji hawahitaji tu kuwa na ustahimilivu wa kipekee, bali pia uwezo wa kimwili wa kukimbia kwa kasi, kubadilisha mwelekeo upesi na kuruka hadi urefu wa ajabu kama ilivyokuwa kwa Cristiano Ronaldo. Zaidi ya hayo, mchanganyiko wa vitu usio na vikwazo vya uratibu na ujuzi wa kipekee wa kukokota mpira huwa ni muhimu kwa mwanasoka ambaye utimamu wake uko imara.

Mahitaji ya kimwili katika kandanda ni tofauti na  huathiriwa na nafasi za wachezaji uwanjani ambapo washambuliaji hutanguliza kasi na wepesi, ilhali mabeki hutegemea nguvu na ustahimilivu.

Hata hivyo, jambo linalofanana kati ya wachezaji wote ni hitaji la kustahimili muda mrefu kukimbia pamoja na uwezo wa kutekeleza ufungukaji kwa kasi pamoja na mabadiliko ya ghafla ya mwelekeo ili kupata fursa za malengo ya uwanjani.

Kufikia stamina na nguvu zinazohitajika kwenye kandanda la daraja la juu hujumuisha mazoezi madhubuti. Wachezaji huwekeza saa nyingi kila siku katika shughuli kama vile kukimbia, kunyanyua vitu vizito na mazoezi maalumu. 

Uangalifu maalumu pia unatolewa katika kuboresha ujuzi wa mpira na kufanya mazoezi ya matukio mbalimbali ya ndani ya mchezo. Mambo hayo yanahitaji mipango kabambe ukiwamo umakini wa upimaji afya kwa wachezaji wa soka. Ikumbukwe mchezo wa soka anahusika kukumbana kimwili, huku pia akitakiwa kuwa na nguvu na kasi.

Uwanjani, hakuna nafasi ya kubadilisha utimamu wa afya, ingawa mchezaji aliyepo benchi anaweza kutulia huku akisoma tu jinsi mwili wake utakavyowakabili wapinzani.

Kutobadilika kwa utimamu wa afya kunamaanisha kwamba wanasoka wengi hucheza mchezo mzima bila mapumziko au kuisha. Hivyo mtaji mkubwa ni afya ya mchezaji iliyotathiminiwa muda mrefu na kuonekana haina shida. Muda wa mapumziko pekee ndio unaotoa ahueni kwa mchezaji. Katika uwanja wa kutosamehe makosa ya kiufundi, kudumisha hali ya juu ya mwili sio faida tu, bali ni ufunguo wa kustahimili matakwa yasiyokoma ya mchezo wa soka.

Hivyo mipango ya utathimini wa afya ya mwanasoka inahitajika kufanyika mapema katika muda sahihi kama ilivyo kipindi ambacho ligi haijakaribia.

UCHUNGUZI WA KIMWILI Kwa wachezaji wa kandanda uchunguzi wa kimwili unajumuisha tathmini zinazofanywa na madaktari na wafanyakazi wa afya.

Vilevile kutathimini utimamu wa mwili, utayari au shughuli nyingine za michezo.  Uchunguzi huo ni muhimu kwa kuzuia majeraha na kutambua hali zinazoweza kuwa hatari kama vile matatizo ya moyo na mishipa ambayo yanaweza kusababisha mshtuko wa ghafla wa moyo na hatimaye kupata ulemavu wa kudumu au kifo cha ghafla.

UCHUNGUZI UKO HIVI Uchunguzi wa kina wa historia ya matibabu ikiwa ni pamoja na majeraha ya awali, mzio wa dawa na historia ya matibabu ya familia hufanyika. Uchunguzi wa kimwili unaolenga kutathmini afya ya jumla, urefu, uzito, shinikizo la damu, kiwango cha mapigo ya moyo, utendaji kazi wa mapafu na mfumo wa misulimifupa.

Vilevile kutambua dalili za majeraha au upungufu wa  kimwili ikiwamo maumivu ya misuli, uvimbe katika mwili, mkwamo wa utendaji kazi wa maungio, dosari kama vile matege au udhaifu wa viungo.

Uchunguzi wa kimaabara ikiwa ni pamoja na hesabu za seli za damu, viwango vya sukari ya damu, wasifu wa lipid ya damu, utendaji kazi wa ini, utendakazi wa figo na zaidi.

tathmini ya mfumo wa moyo na mishipa ili kuhakikisha uwepo wa masuala ambayo yanaweza kusababisha hatari wakati wa shughuli za kimwili. Pia hufanyika tathmini ya afya ya misuli na mifupa, kunyumbulika na aina mbalimbali za mwendo.

Chukua hii Tathmini hizo za afya ya mwili siyo muhimu kwa wachezaji wa kulipwa tu, bali pia kwa wale wengine na vijana ambao wanajiunga katika shule za awali za soka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live