Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Hussein Ali Mwinyi: CCM waliteua mshindi

E6e8d931280a9a797c96750e22d63198 Hussein Ali Mwinyi: CCM waliteua mshindi

Thu, 22 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

JANA katika mfululizo wa makala haya, tulianza kuangalia kwa nini Dk Hussein Mwinyi ni chaguo sahihi la Chama Cha Mapinduzi kugombea urais Zanzibar. Tuliona kwamba mbali na sifa zake binafsi kama za elimu, mvuto, uzoefu wa masuala ya kimataifa lakini pia kuna faida saba za kumteua mgombea huyu.

Baadhi ya faida hizo ni uwezo wake wa kulinda Muungano, kudumisha amani na utulivu Zanzibar, kulinda Mapinduzi na kuleta mageuzi katika visiwa hivyo. Tuendelee kuangalia kwa nini Dk Mwinyi alikuwa chaguo sahihi kugombea urais Zanzibar.

MZIGO WA KUPATA MGOMBEA

Sita, kwa CCM kuteua Hussein Mwinyi, pengine chama kimejipunguzia changamoto, kazi na mzigo wa kupata mgombea wa urais wa Tanzania mwaka 2025.

Pengine historia inaweza kujirudia tena kwa Hussein Mwinyi kufuata nyayo za baba yake kwa kuteuliwa kugombea urais wa Tanzania, baada ya miaka mitano ya kuongoza Zanzibar.

Tunazugumzia 2025, kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, hauwezi kuwa na mshindi mwingine tofauti na Rais John Pombe Magufuli, hata kama utakuwa na wagombea wengi. Huo ndio ukweli wa hali halisi ya sasa.

Shughuli ya kumpata mgombea urais katika Tanzania, na pote duniani kwa jumla, ni shughuli ngumu na yenye kuhitaji umakini mkubwa. Chama, ama nchi, inapobahatika kuwa na mgombea mwenye utayari, mwenye sifa, mwenye uzoefu na mwenye rekodi ya uongozi, hasa kama rekodi yenyewe ni nzuri, ya kutukuka na ya kusifika, basi kazi ya kutafuta mgombea inakuwa rahisi kidogo.

Jambo kubwa na dhahiri kabisa ni kwamba ushindani wa kupata mgombea wa urais wa Tanzania mwaka 2025 utakuwa mkali sana kwa sababu liko rika la wanasiasa vijana wa sasa ambao watakuwa wamekomaa na watakuwa tayari kujipima nguvu kwenye dimba la juu kabisa la kisiasa nchini.

Hivyo, ili mtu apenye, akiwemo Hussein Mwinyi mwenyewe, kama ataamua ama kuombwa kugombea urais wa Jamhuri badala ya kusaka muhula wa pili wa uongozi wa Zanzibar, itakuwa kazi kubwa kweli kweli, na maandalizi yatatakiwa kuwa ya kutosha, ya kisiasa na kisayansi, na ya muda mrefu.

Magwiji wenyewe wa kutengeneza na kuandaa viongozi wakuu (King Makers) ndani ya CCM yenyewe na ndani ya mifumo ya dola, wanajua vizuri zaidi namna ya kuifanya kazi hiyo na sifa zinawaongoza katika kumteua mtu mmoja wa mwisho.

Na bila shaka kazi hiyo kwa mwaka 2025 itakuwa imeanza na inaendelea kwa sababu ya kwao ni kazi ya kudumu, na isiyo na likizo ama ukomo. Anapopatikana mgombea mmoja, mchakato wa kumtafuta mrithi wake, unaanza.

Wao, King Makers, ndiyo wanajua sifa za mtu atakayekuwa anahitajika kuongoza Tanzania ya mwaka 2025 kwenda mbele. Hawa ni sawa na Rain Makers, watengenezaji mvua, sifa na mbinu za kazi zao wanazijua wenyewe. Kwetu sisi, tunabakia kubashiri tu. Na mimi nitajaribu kushiriki ubashiri hapa.

Kwa uzoefu wa kihistoria, utamaduni na siasa za Chama Cha Mapinduzi na Tanzania kwa jumla, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano mwaka 2025, kama halitafanyika jaribio la kubadilisha Katiba, kwa sababu Afrika yetu huendeshwa kwa konakona nyingi, atakuwa na baadhi ya sifa zifuatazo:

Pengine atakuwa Muislamu baada ya miaka 10 ya uongozi wa Mkristo. Pengine atatoka Zanzibar kwa sababu itakuwa imepita miaka 30 tangu upande wa Zanzibar wa Muungano wa Tanzania kutoa kiongozi mkuu wa taifa, mwaka 1985, katika nafsi ya Ali Hassan Mwinyi.

Kwa utaratibu wa CCM usioandikwa popote, atakuwa mdogo kwa umri, mwenye miaka kati ya 55 na 60, kuliko Rais atakayekuwa anaondoka madarakani – Rais Magufuli, ambaye atakuwa na umri wa miaka 68 hivi. Yaani atakuwa kijana zaidi kwa Magufuli, kwa angalau, miaka kati ya mitano na kumi.

Ni lazima awe na uzoefu wa kutosha wa Serikali kwenye nafasi ya Waziri ama juu ya hapo. Ni lazima awe na sifa za kuaminika na zilizothibitika za uongozi.

Zipo sifa mbili nyingine kubwa za ziada. Ni lazima akubalike ndani ya CCM na akubaliwe na wana-CCM. Awe mwenzao, kwa kutumia lugha yao wenyewe. Hawa wanayo tabia ya kuangaliana machoni, kama siyo mwenzao na hawakuamini, hawakuchagui, hata uwe na sifa nyingi kiasi gani.

Na mwisho ni lazima aweze kukabiliana na kuwashinda wapinzani katika mfumo wa siasa za vyama vingi. Hii ina maana kuwa lazima awe na mizizi ya kisiasa ya nguvu Tanzania Bara, mbali ya Zanzibar.

Mwaka 2025, kama ilivyo sasa, wenye sifa zilizotajwa hapo juu watakuwa wengi. Wanasiasa vijana Wazanzibari watakuwa wengi pia. Aidha, wanasiasa Wazanzibari Waislamu watakuwa wengi kwa sababu katika Zanzibar kiongozi adimu ni Mkristo, si Mwislamu.

Jambo gumu, hata hivyo, litakuwa ni kumpata mwanasiasa mgombea kwenye sifa binafsi kama zile za Hussein Mwinyi zilizotajwa mwanzoni mwa makala haya. Lakini gumu zaidi, itakuwa ni kumpata mgombea mwenye sifa ya kuwa ameongoza Zanzibar na kupata uzoefu wa uongozi wa ngazi hiyo ya juu kwa miaka mitano tayari.

RIKA JIPYA LA UONGOZI

Saba, mwisho kwa CCM kumteua Hussein Mwinyi kugombea Urais wa Zanzibar, chama hicho kimeendeleza utamaduni wa ujenzi mpya wa tabaka na rika jipya la viongozi wakuu.

Hata kama ubashiri ulioelezwa hapo juu, hautakuja kutokea kama ulivyoelezwa, bado Chama Cha Mapinduzi kimeanzisha safari nyingine ya kujenga tabaka na rika la makada vijana kuingia katika uongozi wa juu wa nchi.

Dk Hussein Mwinyi siyo wa kwanza, wala pekee, katika safari ya ujenzi huo. Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, ni mwingine, na Baraza la Mawaziri limejaa vijana kibao wazuri na wenye sifa kemkem.

Tofauti na vyama vingine ambavyo vingi ni vichanga na vipya, havina uzoefu wa kisiasa wala uongozi, CCM imekuwa katika mchezo huo kwa miaka mingi, tangu kwenye miaka ya 1950, wakati kilipoundwa Chama cha Uhuru wa Tanganyika cha Tanganyika African Union (TANU) mwaka 1954, na Chama cha Mapinduzi ya Zanzibar cha Afro-Shiraz Party, mwaka 1957, vyama mama vya CCM.

Kwa sababu hizo za kihistoria zilizoambatana na sera nzuri na uongozi safi wenye visheni na maono thabiti, CCM imejenga uwezo wa kuandaa na kuwa na kundi kubwa la makanda kwenye ngazi za juu za uongozi, na hivyo kuwa na wigo mpana zaidi wa kutafuta kiongozi wa juu muda unapofika.

Wenzao katika vyama vingine, mambo bado kabisa, na ndiyo maana vikipata kiongozi mmoja vinamshikilia na kumruhusu kugombea uongozi wa juu wa nchi mara nyingi kupita kiasi, hata kama wenzake ndani ya chama wanajua fika kuwa hawezi kushinda.

Na mara nyingi, kiongozi huyo anaishia kukiongoza chama katika njia isiyo, kwa vile mawazo yanachoka na nguvu inaisha. Kwake, uongozi badala ya kuwa dhamana, unakuwa kazi.

Mifano iko wazi: Seif Sharrif Hamad amekuwa anagombea Urais wa Zanzibar tangu 1995 wakati ulipoanzishwa mfumo wa vyama vingi. Profesa Ibrahim Lipumba naye amegombea Urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995 akichuana na Marehemu Mzee Benjamin Mkapa.

Wote wawili wameendelea kugombea na bado wanagombea nafasi hizo hizo mwaka huu. Waliposhindwa kuzipata nafasi hizo huko nyuma, wakaamua kukabiliana wenyewe, ana kwa ana, kugombea nani zaidi ndani ya CUF. Matokeo yake, chama kimebakia vipande vipande, kinapumulia mashine, Waswahili wanasema.

Hata kiongozi awe mzuri kiasi gani, kukaa madarakani kupitiliza ni tatizo kubwa kwa nchi, na kwa maendeleo ya wananchi, hata kama yeye anaendelea kufaidi uongozi.

Historia iko wazi; kwa kadri kiongozi anavyozidi kukaa madarakani, ndivyo mambo yanavyozidi kuharibika. Bara la Afrika, hasa, limejaa mifano mingi ya jambo hilo, tukianzia na baadhi ya nchi zinazotuzunguka.

Mawazo mapya yanaanza kuwa adimu, na hatimaye yanakauka kabisa; uongozi unaendeshwa kwa mazoea, na pengine kwa ubabe bila kujali maslahi ya watu; madaraka na mamlaka ya kweli kweli kutoka kwa wananchi yanapungua, na kiongozi anabakia amezungukwa na vibaraka wakizidi kumdanganya, kwa nia moja tu – kupata vyeo na kujinufaisha binafsi.

Matokeo yake, kasi ya nchi kusonga mbele inasimama na kudumaa, na maendeleo yanadorora kabisa, mpaka kiongozi wa namna hiyo aondolewe madarakani, kwa namna moja ama nyingine, kwa njia ya amani (kama ipo), ama kwa nguvu na mabavu, kama tulivyoona katika nchi za Afrika Magharibi ya Mali majuzi.

Katika uhai wake, CCM imejitahidi kuepuka hali hiyo kwa kuwa na sera nzuri na kujenga taratibu nzuri ikiwemo ya kuendesha chaguzi za mara kwa mara, kila baada ya miaka mitano na kwa viongozi kung’atuka madarakani muda wap unapomalizika.

Mfumo huu si tu unakiwezesha chama hicho kupata viongozi wapya, vijana zaidi, wenye fikra na mawazo mapya kusukuma mbele vyombo vya uamuzi, lakini pia inasaidia kujenga uendelevu wa chama chenyewe na sera zake.

Kwa CCM yenyewe, hiyo ndiyo maana kubwa, na ya mwisho, ya uteuzi wa Hussein Ali Mwinyi kugombea Urais Zanzibar.

Mwandishi wa makala haya ni miongoni mwa waandishi nguli nchini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu (mstaafu).

Chanzo: habarileo.co.tz