Sakata la beki Lameck Lawi limeibua sura mpya baada ya kuelezwa kuwa huenda mchezaji huyo akarudi nchini kutokana na dili lake na K.A.A Gent ya Ubelgiji kuingia mchanga huku mwenyewe akifunguka hali ilivyo.
Ipo hivi; Lawi alikuwa anahitajika na timu hiyo kwa makubaliano ya kumnunua moja kwa moja lakini mara baada ya kufika Ubelgiji mambo yamekuwa tofauti.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal Union kimeliambia Mwanaspoti kuwa, K.A.A Gent imeahirisha mpango wa kumnasa beki huyo hivyo wanafanya mpango wa kumtafutia timu nyibgine ili afanye majaribio.
“Lawi alikuwa anaenda kujiunga moja kwa moja na K.A.A Gent kutokana na timu hiyo kuwa na mpango wa kumuuza beki wao wa kati lakini biashara hiyo haijafanyika hivyo hawaoni umuhimu wa kubaki naye kikosini,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Kwa sababu hakukuwa na makubaliano ya majaribio kati ya mchezaji wetu na timu hiyo tumeona ni bora mchezaji huyo atafutiwe timu yoyote nchini Ubelgiji na sio masuala ya majaribio, ikishindikana atarejea nchini.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta Lawi ambaye alisema haelewi ishi hiyo huku yeye akiendelea kufanya mazoezi na timu ya K.A.A Gent.
“Mimi kazi yangu ni kucheza, kuhusiana na masuala ya kuuzwa, kutolewa kwa mkopo au kufanya majaribio hilo viongozi ndio wanaelewa, mimi nipo huku kufanya kazi yangu uwanjani,” alisema na kuongeza;
“Tangu nimetua huku nimekuwa nikifanya mazoezi na timu, ukiniuliza masuala ya kufanya majaribio siwezi kuwa na jibu sahihi, viongozi wangu ndio wanatakiwa kutoa ufafanuzi.”
Beki huyo ambaye alifanya vizuri msimu uliopita akiisaidia timu yake kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, licha ya kutimkia Ubelgiji alikuwa anahusishwa kumalizana na Simba.