Nigeria na Kenya zinaongoza barani Afrika kwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha kutoka kwa raia wao walioko ughaibuni (Diaspora). Mithili ya maji yatiririkayo kwenye ardhi kame, Dola za diaspora, zinachangia sehemu muhimu katika maendeleo, kupunguza umaskini, katika hili kuna mambo muhimu kujifunza kwa nchi yetu.
Taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu mwenendo wa uhamiaji duniani (KNOMAD, 2024) inaonesha kuwa kufikia Desemba 2023, Diaspora wa Nigeria walituma kiasi cha dola bilioni 19.5 kwa nchi hiyo, ikiwa ndio kiwango kikubwa zaidi barani Afrika. Kiasi hiki ni zaidi ya robo ya jumla ya dola bilioni 54 zilizopokewa na nchi 49 za ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kwa Nigeria, sababu kubwa ni kuwa na idadi ya raia wengi wanaoishi au kufanya kazi nje ya nchi, wanaweza kuwa raia wa Nigeria au wenye asili ya nchi hiyo. Miongoni mwao wapo wenye ujuzi wa kitaalamu ambao wamepata nafasi katika soko la ajira ughaibuni.
Kwa Afrika, michango ya diaspora ni muhimu sana na inaweza kuzidi kiasi cha mikopo au misaada ya kimataifa kwa mwaka. Kwa mfano, nchini Nigeria, mwaka 2022, fedha zilizotumwa na diaspora zilifikia dola bilioni 25, sawa na asilimia 6.1 ya Pato la Taifa (GDP). Kwa ulinganisho, kiwango hiki kilikuwa kikubwa zaidi kuliko jumla ya fedha za uwekezaji wa kigeni (FDI) na misaada.
Inaelezwa kuwa mkakati wa kisera kuratibu diaspora unachangia pakubwa mafanikio hayo ya Nigeria. Mathalani, Tume ya Nigeria ya Diaspora (NiDCOM), iliyoanzishwa mwaka 2017, inaratibu shughuli za diaspora, kutoa fursa, mwongozo na kuhakikisha utumaji wa pesa unalenga kuwekeza sambamba na malengo ya maendeleo ya kitaifa.
Mojawapo ya mbinu iliyobuniwa ni kuanzisha hati fungani ya diaspora mwaka 2017, ambapo mwanadiaspora anaweza kutuma fedha kununua hati fungani nchini kwao. Fedha zinazokusanywa kupitia hati hizi zinaelekezwa moja kwa moja kwenye miradi ya miundombinu, kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Kwa Afrika Mashariki, Kenya inaongoza kwa kupokea dola za diaspora. Mwaka 2023, inakadiriwa ilipokea dola bilioni 4.2 kutoka kwa raia wake walioko ughaibuni, kiwango hicho ni zaidi ya mapato ya mauzo ya nje katika sekta za utalii, chai, na kahawa, ambazo zilipata jumla ya dola bilioni 1.2 (KNOMAD, 2024).
Ufanisi wa Kenya unachangiwa na maendeleo ya teknolojia ya malipo na utumaji fedha kidijiti, ambayo imeongeza kasi na kupunguza urasimu katika kupokea fedha kutoka nje. Kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Kenya kuhusu mwenendo wa utumaji fedha (Kenya Diaspora Remittances Survey, 2021), asilimia 72 ya fedha zinazotumwa Kenya hupokewa ndani ya siku moja.
Vilevile, sehemu kubwa ya raia wa Kenya walioko ughaibuni ni wenye elimu ya juu, ripoti inaonesha asilimia 60 yao wanamiliki shahada za vyuo vikuu na hufanya kazi za staha, hususan katika nchi za Ghuba, Ulaya, na Amerika Kaskazini.
Hata hivyo, nchi za Afrika zinahitaji kuboresha mifumo yake ili fedha za diaspora ziingie kwenye mifumo rasmi ya kibenki au malipo, na kuongeza faida za kiuchumi kama kuratibu hifadhi ya fedha za kigeni.
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa Mataifa yaliyopo kusini mwa Jangwa la Sahara yana gharama kubwa zaidi za kutuma pesa duniani. Kwa mfano, kutuma dola 200 hugharimu wastani wa asilimia 7.9, kiwango kikubwa zaidi ikilinganishwa na Amerika ya Kusini (5.9%), Asia ya Kusini (5.8%), na Ulaya na Asia ya Kati (6.7%).
Kwa Tanzania, ambayo ilipokea makadirio ya dola milioni 700 (Sh1.75trilioni) kutoka kwa diaspora mwaka 2023, bado kuna changamoto ya kupunguza gharama za kutuma fedha. Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zenye gharama kubwa za kutuma fedha.
Hata hivyo, ipo haja ya kuendeleza mikakati inayoratibu na kurahisisha ushiriki wa makundi ya diaspora katika shughuli za kimaendeleo na uchumi kupitia majukwaa maalumu.