Sergio Ramos Garcia licha ya kwamba alizaliwa na kuanza maisha yake ya soka ndani ya Klabu ya Sevilla lakini ni moja ya wachezaji wanaoheshimika vilivyo Real Madrid.
Heshima ya Ramos Madrid inakuja kwa sababu ya kuiongoza katika mafanikio makubwa akiwa mchezaji wa kawaida na hata pale alipokuwa nahodha akipokea kitambaa kutoka kwa Iker Casillas mwaka 2015.
Tangu wakati huo hadi msimu wa 2021/22 alipoondoka Madrid, Ramos alibeba mataji 12, yakiwemo matatu mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 'Uefa'.
Hapo pia usisahau kuna Ligi Kuu Hispania 'La Liga', Supercopa de Espana, Kombe la Dunia la Klabu na Uefa Super Cup.
Mataji hayo yamemfanya Ramos kuwa moja ya manahodha wa Real Madrid waliobeba mataji mengi hadi alipoondoka na kuhamia Paris Saint-Geirman ya Ufaransa.
Kwa hapa Bongo, tuna Sergio Ramos wetu na anapatikana mitaa ya Twiga na Jangwani ilipo klabu ya Yanga. Wawili hao kwa maana Ramos wa Ulaya na huyu wa Tanzania wote walihamia klabu ambazo zimewapa heshima ya kubeba mataji mengi.
Ramos wa Bongo ardhi ya Julius Nyerere ni Bakari Nondo Mwamnyeto, ni mmoja wa manahodha waliobeba mataji mengi tangu alipowasili kwa Wananchi Agosti Mosi mwaka 2020.
Mwamnyeto alitua Yanga akitokea Coastal Union ya Tanga alikozaliwa na kazi kubwa aliyoifanya ndani ya kikosi hicho ndiyo iliwashawishi mabosi wa Yanga kuvunja benki na kuinasa saini yake na kumfanya kuwa beki mzawa aliyesajiliwa kwa kitita kikubwa zaidi kikitajwa kufikia milioni 200.
Beki huyo awali alikuwa anatajwa kutua Simba lakini matajiri wa Jangwani walifanya umaafia kwa kunasa saini yake akiwa njiani kuja Dar es Salaam tayari kwa kumalizana na Wanamsimbazi.
Inaelezwa kigogo mmoja wa Yanga alimfuata Mwamnyeto akiwa Morogoro kwa ajili ya kuja Dar es Salaam na kumbadilishia uelekeo wa kwenda kumalizana na Simba badala yake akatua Jangwani.
Beki huyo alikabidhiwa unahodha wa Yanga akichukua kitambaa kutoka kwa beki mwenzake, Mghana, Lamine Moro ambaye aliachwa na klabu hiyo baada ya pande mbili kukubaliana kuvunja mkataba ikiwa ni baada ya kudumu kwa miaka miwili.
Tangu Mwamnyeto abebe kitambaa hicho cha unahodha wa Yanga hadi sasa amebeba mataji 11 ambayo yanamfanya kuwa miongoni mwa manahodha ambao wamechukua mataji mengi.
Hadi sasa katika kabati la Mwamnyeto ana makombe ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho, Ngao ya Jamii, Kombe la Mapinduzi na kombe la Toyota Super Cup alilolibeba Afrika Kusini wakati wa maandalizi ya kujiandaa na msimu.
Mwamnyeto amebeba mataji hayo na matatu ni ya ligi kuu, matatu ya Kombe la Shirikisho na Ngao tatu. Beki huyo amebeba Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho kwa misimu mitatu mfululizo kuanzia msimu wa 2021/22 hadi msimu uliopita wa 2023/24.
Pia nahodha huyo aliiongoza klabu hiyo kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2021 Zanzibar baada ya kuwafunga Simba kwenye penalti 4-3.
Usisahau beki huyo ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Tanga ameshinda Ngao mbili za Jamii katika mwaka 2021 na 2022 ambazo zote waliwafunga watani zao Simba kwa bao 1-0 na 2-1.
Katika mechi hizo mabao ya Yanga yote yalifungwa na straika Mkongomani, Fiston Mayele ambaye kwa sasa yuko Misri katika klabu ya Pyramid.
Pia Ramos huyo wa Bongo amebeba Ngao ya Jamii juzi Jumapili walipoichapa Azam FC kwa mabao 4-1 katila mchezo wa fainali kama ambavyo waliwafanyia Wasauzi, Kaizer Chiefs katika kombe maalumu la michuano ya kujiandaa na msimu la Toyota Cup.
Beki huyo kwa sasa amekuwa hana nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Yanga mara kwa mara kutokana na uwepo wa mabeki wenzake, Dickson Job na Ibrahim Hamad 'Bacca' ambao wamekuwa chaguo la kwanza la kocha Miguel Gamondi.
Licha ya hivyo, hilo halimuondolei heshima ya kuwa nahodha wa Yanga ambaye amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kama ilivyowahi kuwa kwa nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nadir Haroub 'Cannavaro'.
Mwamnyeto kwa msimu pia ana nafasi kubwa ya kuongeza rekodi yake hiyo ya kubeba mataji kutokana na timu yake kuwa na kikosi kikali ambacho kinapewa nafasi kubwa ya kuchukua mataji hii ni baada ya kuongeza mkataba wa kuendelea kusalia Jangwani kwa misimu mingine miwili.
Kama umesahau, Mwamnyeto pia ndiye nahodha wa Yanga aliyeiongoza timu hiyo kubeba medali ya mshindi wa pili wa Kombe la Shirikisho Afrika misimu miwili nyuma timu yake ikicheza hatua ya fainali baada ya miaka 25.
Mbali na hilo pia msimu uliofuata alikiongoza kikosi cha Yanga kucheza hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika, Kwa hakika huyu ni Sergio Ramos halisi wa Bongo kwa nafasi ambazo wanacheza na mataji waliyobeba.
MSIKIE MWENYEWE
Mwamnyeto anasema kila mchezaji anatamani kufikia mafanikio ya kutwaa mataji mwisho wa msimu na kwake ni faraja kubwa kucheza timu ambayo anaiongoza kwa kuvaa kitambaa ikiwa na mafanikio makubwa.
“Nimeweka rekodi nzuri ambayo hata kizazi changu sitakuwa na maneno mengi kuwaambia kuhusu upambanaji wangu kwenye masuala ya soka, medali pekee zitatoa picha ya ubora wangu,” anasema na kuongeza;
“Mafanikio niliyoyapata Yanga ni misingi imara niliyojijengea kwa kuhakikisha nasaidiana na wenzangu kupambania timu ifikie mafanikio, ushirikiano mzuri baina ya wachezaji na benchi la ufundi ndiyo siri ya mafanikio.”
Mwamnyeto anasema baada ya kuanza msimu kwa kutwaa taji la ngao wanawekeza nguvu zao kwenye michuano ya ligi kuu, Kombe la Shirikisho la Azam na Ligi ya Mabingwa Africa kote wakiwa na malengo sawa kuhakikisha wanakuwa bora na kufikia mafanikio.