Idadi ya timu sita zinazoshiriki mashindano ya klabu Afrika yatakayoanza mwishoni mwa wiki hii zitatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zao za nyumbani.
Sababu tofauti zimechangia kuzifanya timu hizo kuchagua uwanja huo unaomilikiwa na Azam FC ambazo ni usalama duni katika baadhi ya nchi ambazo timu hizo zinatoka na pia timu nyingine kukosa viwanja vinavyokidhi vigezo vya kutumika kwa mashindano hayo.
Timu hizo saba ambazo zitatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi za mashindano ya klabu Afrika msimu huu ni wenyeji Azam FC, Dekedaha, Arta Solar, Horseed, Rukinzo na Coastal Union.
Hali hafifu ya kiusalama katika nchi ya Somalia imelazimisha mabingwa wa nchi hiyo kuomba kutumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi yake ya nyumbani ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Arta Solar ya Djibouti, Agosti 23.
Mchezo huo utakuwa ni wa marudiano na mechi ya kwanza ambayo itakuwa Agosti 16, itachezwa katika uwanja huohuo kwa vile Arta Solar nayo imepanga kutumia Azam Complex kwa mechi zake za nyumbani.
Uamuzi wa Arta Solar kucheza Azam Complex umetokana na sababu ya kukosekana kwa uwanja unaokidhi vigezo vya kuandaa mechi za mashindano ya klabu Afrika nchini kwao Djibouti.
Timu mbili za Burundi nazo zitatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zao za nyumbani kutokana na nchi yao kutokuwa na uwanja stahiki wa kuandaa michezo ya kimataifa.
Mabingwa wa Burundi, Vital’O watakabiliana na Yanga katika mechi yao ya nyumbani ya Ligi ya Mabingwa Afrika uwanjani hapo, Agosti 17.
Rukinzo ya Burundi inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika pia itacheza Azam Complex katika mechi yake ya nyumbani dhidi ya Horseed ya Somalia, Agosti 23. Ikumbukwe Horseed nayo inatumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zake za nyumbani za mashindano hayo.
Wawakilishi wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Coastal Union nao watacheza mchezo wao wa nyumbani wa hatua ya kwanza ya mashindano hayo dhidi ya Onze Bravos ya Angola katika Uwanja wa Azam Complex.
Timu ya saba ambayo itautumia Uwanja huo ni mwenyeji Azam FC ambayo katika Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa kuanza dhidi ya APR ya Rwanda, Agosti 18 uwanjani hapo na mechi ya marudiano itakuwa ni huko Kigali, Rwanda Agosti 24.