Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems: Sasa Singida Black Stars imekwiva

Patrick Aussems FIFA.jpeg Patrick Aussems.

Thu, 25 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, Mbelgiji Patrick Aussems amesema kwa sasa ameridhika na viwango vya wachezaji wake, huku akiweka wazi kambi ya kikosi hicho iliyopo jijini Arusha imekuwa na manufaa makubwa tangu wamewasili.

Kauli ya Aussems inajiri baada ya timu hiyo kucheza michezo miwili ya kirafiki ya kujipima ubavu jijini humo ikianza na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Polisi Tanzania kisha kutoka sare ya 2-2 na ACA Eagles, ikiwa ni siku kadhaa tangu ilipong’olewa katika michuano ya Kombe la Kagame 2024 iliyomalizika wikiendi iliyopita.

“Sio rahisi kutengeneza muunganiko kwa haraka kwa sababu wachezaji wengi ni wapya na hawajazoeana ila kuna maendeleo ya mmoja mmoja ambayo tunayaona, kikubwa kama benchi la ufundi ni kuwaunganisha ili kupata kilichokuwa bora kwao,” alisema Aussems.

Aussems aliongeza, jambo kubwa linalompa matumaini ni jinsi wachezaji wanavyojituma hali inayowapa ari na motisha ya kuamini msimu ujao watafanya vizuri zaidi kwa sababu ya ubora na uwezo wa nyota waliopo kikosini humo.

Kwa upande wa nyota wa kikosi hicho, Edmund John aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Geita Gold alisema, suala la ushindani wa namba limekuwa kubwa kwao, kwa sababu kila mchezaji anataka kupambana ili kushawishi benchi la ufundi.

“Singida ni timu yenye malengo makubwa ndiyo maana hata wachezaji waliopo hapa ni wakubwa na wenye uzoefu, ushindani ni mzuri kwa sababu kadri unavyopambana na aliyekuwa juu yako inakufanya pia nawewe kuzidi kuongeza juhudi,” alisema.

Aussems aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali ikiwemo Simba, alianza kukifundisha kikosi hicho katika michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika Jumapili iliyopita, ambapo alishindwa kutamba na kutolea hatua ya makundi.

Singida ilikuwa Kundi C na ilimaliza nafasi ya tatu na pointi tatu nyuma ya vinara APR ya Rwanda iliyomaliza na pointi saba, huku SC Villa ya Uganda ikishika ya pili na pointi tano wakati Al-Merrikh ya Sudan Kusini iliburuza mkia na pointi moja.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live