Rais Museveni amesema kuwa sio mara ya kwanza kwake kushiriki ujenzi wa shule nchini Tanzania, kwani ameshafanya hivyo mara mbili kwa kujenga shule za msingi ambazo zinatumika hadi hivi sasa japo alipinga kutumika kwa jina lake katika taasisi zozote zile ndani na nje ya nchi ya Uganda.
Ametoa kauli hiyo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu ombi la Hayati Maghufuli la mwaka 2019 wakati alipofanya ziara nchini Tanzania. amesema kuwa hapo awali aliomba kujenga shuleni kwa hiari yake, lakini awamu hii aliombwa kujenga kwani Hayati Maghufuli alikuwa akitambua nia yake katika kuboresha miundombinu ya elimu.
Amesema kuwa kitendo cha Hayati Maghufuli kumuomba ajenge shule hiyo hakimaanishi kuwa Serikali ya Tanzania haikuwa na uwezo wa kujenga shule hiyo ambayo imegharimu dola za kimarekani milioni 1.67 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 3.841.
Museveni amesema kuwa, Mwaka 1969 wakati wa kupigana vita na Idi Amini wakiwa wamejificha mkoani Kagera walifika katika moja ya shule ambayo mazingira yake hayakuwa vizuri hivyo alimuomba Hayati Nyerere ampe ruhusa kujenga shule ambayo itatumika kama kumbukumbu.
Akizungumza kuhusu kutumika kwa jina lake kama ambavyo majina ya marais wengine yakitumika, amesema kuwa yeye alishapinga jina lake kutumika katika ulimiliki wa mali ambazo sio zake, jambo ambalo limepelekea hadi hivi sasa katika kipindi chote alichoongoza taifa la Uganda kuwa hakuna mahali jina lake linatumika nje na matumizi ya kifamilia.
"Hii ndo mara ya kwanza duniani kupatikana kwa taasisi inayoitwa Yoweri museveni, haijawahi kuwepo, na hijawahi kuwepo kwasabu kule Uganda nilishapiga marufuku jina langu kutumika kwenye mali za watu, hapa nawasaidia kumaliza shida zenu nikimaliza narudi kwenye ng'ombe zangu, hakuna kinachotumia jina langu zaidi ya mke wangu na watoto wangu, ila hapa Tanzania wameamua na siwezi kuwapinga kwa hili" Amesema Museveni.