Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Simbachawene ashangaa Watanzania kutumia mkaa, kuni

86497 Pic+simbachawene Waziri Simbachawene ashangaa Watanzania kutumia mkaa, kuni

Fri, 29 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya teknolojia mbalimbali za nishati jadidifu kuibuliwa, Watanzania wameendelea kuwa wagumu kutumia bunifu hizo.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Novemba 29, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira nchini Tanzania, George Simbachawene wakati akifungua maonyesho ya siku mbili ya nishati jadidifu yaliyohusisha wavumbuzi na kampuni 23 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kumaliza kutembelea mabanda ya maonyesho kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam, Waziri Simbachawene amesema anashangaa kuona Watanzania bado wanatumia mkaa na kuni wakati kuna majiko yanayotumia nishati mbadala.

Amesema matumizi ya mkaa na kuni yameendelea kuwa kikwazo kwenye mazingira na kuleta athari mbalimbali.

“Nimeona kuna teknolojia nyingi, majiko ya kila aina tena yanatumia nishati mbadala lakini watu bado wanang’ang’ania mkaa na kuni.”

“Tunaposema kuna mabadiliko ya tabia nchi ukweli ni kwamba yanasababishwa na hivi vitu tunavyotumia. Niwasihi Watanzania tubadilike tutumie majiko haya ya nishati jadidifu,” amesema

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Nishati Jadidifu (Tarea), Prosper Magali amesema wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuhakikisha wanabuni nishati mbalimbali hasa kwa wananchi wa vijijini.

Amesema maonyesho hayo yatatoa fursa kwa wananchi kujionea mambo yanayohusu nishati jadidifu na teknolojia zake.

Magali amesema teknolojia za nishati jadidifu zikitumika itasaidia kupunguza kiwango cha ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa huku akieleza kwa mwaka Tanzania zinatumika tani milioni mbili za mkaa.

Chanzo: mwananchi.co.tz