Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Simbachawene afunguka zuio mikutano

97399 Pic+simbachawene Waziri Simbachawene afunguka zuio mikutano

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema hana maelekezo ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Akizungumza na Nipashe jana katika mahojiano maalum kuhusu mikutano ya vyama vya siasa kama inaruhusiwa kufanyika au la kuelekea Uchaguzi Mkuu, Waziri Simbachawene alisema: “Sina maelekezo ya kuzuia mikutano ya vyama vya siasa kwa sababu sijawahi kupewa hicho kitu.

“Bali, Jeshi la Polisi linaweza kutoa kibali cha mikutano pale ambapo hakuna hofu ya uvunjifu wa amani, kama ipo basi linaweza lisitoe likaelekeza vinginevyo.”

Alisema hilo linathibitiwa na sheria nyingine, lakini wao kazi yao ni kutoa vibali kwa mtu anayeona anataka kufanya shughuli yoyote ya mikusanyiko ya watu.

“Ukitaka kufanya shughuli yoyote ya mikusanyiko ya watu kama injili, chama cha siasa au wafugaji wa ng’ombe au walina asali, sisi kazi yetu ni kutoa kibali pale tunapohisi kuna tishio la uvunjifu wa amani linaloweza kutokea kutokana na jambo hilo tunaweza kuzuia na kuelekeza vinginevyo.

Alipoulizwa kuhusu vibali ambavyo vimeshatolewa hadi jana kwa ajili ya mikutano ya vyama vya siasa, Waziri Simbachawene alisema hivi karibuni hawajapata maombi yoyote.

“Wapeleke maombi ya kufanya mikutano Jeshi la Polisi na jeshi litaangalia kama wanaruhusiwa kufanya kwa maana hakuna tishio lolote la uvunjifu wa amani wanaweza kuruhusiwa,” alisema.

Kuhusu Jeshi la Polisi lilivyojiandaa kwenye ulinzi na usalama wakati wa uchaguzi, alisema wakati wote wamekuwa wakifanya hivyo siyo tu kwenye uchaguzi.

“Wakati wote tumekuwa tukihakikisha ulinzi na usalama unaokuwapo, tunahakikisha shughuli zote za maendeleo zinafanyika bila shida, ikiwamo uchaguzi.

“Nikisemea uchaguzi peke yake ni kama ni jambo mahsusi sana katika muhktadha mzima wa amani na utulivu katika nchi, niseme tu kwamba Jeshi la Polisi wakati wote tupo imara kuhakikisha nchi ipo salama ndani ya mipaka na wananchi wanaendelea kufanya shughuli zao.”

Hata hivyo, alisema kuelekea uchaguzi mkuu, wananchi wawe watulivu kwa sababu Jeshi la Polisi limejipanga vizuri kuhakikisha unafanyika salama.

Baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, serikali ilizuia mikutano ya kisiasa, isipokuwa kwa madiwani na wabunge ambao waliruhusiwa kufanya hivyo katika maeneo yao.

Hata hivyo, vyama vya siasa hivi karibuni vimeanza kulalamikia kuendelea kuwapo zuio hilo wakati umebaki muda mfupi wa kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live