Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. George Simbachawene,amesema bado yapo malalamiko mengi ya wananchi kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika ofisi za umma hali inayosababisha wengi wao kushindwa kuzifikia huduma wanazozihitaji.
Waziri Simbachawene,ameyasema hayo leo Novemba 20,2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) unaofanyika kwa siku tatu jijini Dodoma.
Waziri Simbachawene amesema kuwa rushwa ndogondogo bado zipo na zinawakera wananchi hivyo lazima kuwa na mikakati ya kuhakikisha zinazuiliwa.
“Bado suala la rushwa ndogondogo ni tatizo sana kwa wananchi wetu na huko ndiko yapo malalamiko mengi ya watu kutokana na rushwa hiyo kuwanyima fursa ya kupata huduma.
“Huduma hizo ni pamoja na elimu ngazi za chini kati hadi vyuo vikuu, lakini pia huduma za afya,kodi na leseni ambako kumewekwa utaratibu mgumu na ukilitimba katika utoaji wa huduma ili tuu watu watoe rushwa ndipo wahudumiwe”amesema Mhe. Simbachawene
Aidha amesema kuwa kuna haja ya kutengeneza sheria za kuwashughulikia viongozi walioshiriki katika masuala ya rushwa wanapostaafu ili kutoa funzo kwa viongozi wengine.
”Mtu anapostaafu kama alishiriki katika uozo lazima ashughulikiwe tukifanya hivyo tutakuwa tunatoa somo kwa viongozi wengine.Tusipo shughulikiana tutakuwa hatusemi ukweli kwa Taifa letu kwasababu rushwa bado ni tatizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU CP Salum Rashid Hamduni, amesema kuwa katika mwaka wa fedha uliopita taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa sh. bilioni 171.9
“Mafanikio tuliyoyapata katika mwaka wa fedha uliopita TAKUKURU kwa kutumia vyombo vya uchunguzi imefanikiwa kuokoa zaidi ya sh.bilioni 171 fedha hizo kama zisingefuatiliwa zingeishia mikononi mwa watu na kufanyiwa ubadhilifu,”amesema CP Hamduni
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bi.Rosemary Senyamule,amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha uongozi imara kwa vitendo.
“Tunampongeza Rais Dk.Samia kwa kuendelea kuonyesha uongozi imara kwa vitendo ambapo amekuwa akiongeza bajeti ya taasisi hizi zinazosimamia haki na demokrasia ili zifanye kazi kwa weledi,”amesema.