Serikali imesema, mauaji ya wazee yamelitia doa kubwa Taifa na kwamba ni wakati sasa kwa jamii kupambana na kuhakikisha wanazuia.
Kauli hiyo imetolewa jana Oktoba 3, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, George Simbachawene wakati akifunga kilele cha siku ya wazee duniani ambayo Kitaifa sherehe zimefanyika Dodoma.
Simbachawene amesema kitendo cha kuwaua wazee kwa imani za kishirikisha na kw akuwahisi wachawi kutokana na macho kuwa ni mekundi si kitendo cha kiungwana hata kidogo na hakipaswa kuungwa mkono.
Hata hivyo alisema katika kipindi cha mwaka jana Tanzania ilishuhudia amani ikitawala hatukuwa na matukio ya mauaji, lakini mwaka 2022 tena tumeingia kwenye rekodi hiyo mbaya kutokana na matukio yaliyotokea,” amesema Simbachawene.
Waziri amesema ni jukumu la jamii kuwalinda na kuwatunza wazee kwa namna yoyote bila kuwaachia wengine lakini akasisitiza umoja kwa familia kuwatunza wasiojiweza.
Simbachawene amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya kuwapatia vitambulisho wazee katika maeneo yao haraka na kwamba wasiwe na visingizio kwani jambo hilo ni la muda mrefu.
Waziri huyo amesema kuanza sasa hakuna visingizio badala yake Wakurugenzi wawe na utashi wakitambua kuwa kundi hilo linahitaji huduma muhimu mahali popote na wakati wowote.
Kingine amewaagiza vyombo vya ulinzi kusimamia kikamilifu katika suala la ulinzi kwa kundi hilo ambalo limekuwa na malalamiko kwa muda mrefu wakitaja kuonewa.