Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri Mkenda aunda timu kuchunguza utoaji mikopo elimu ya juu (+Video)

Video Archive
Sun, 31 Jul 2022 Chanzo: Mwananchi

Wakati dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2022/2023 likiwa wazi kwa muda wa siku 70 kuanzia Julai 19 hadi Septemba 30 mwaka huu, Serikali imetangaza timu ya watu watatu kuchunguza utoaji wa mikopo.

Akitangaza timu hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema itaongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dk Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu.

Profesa Adolf Mkenda amesema timu hiyo itachunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo kwa watu wasiokuwa na sifa.

Amesema timu hiyo itapitia malalamiko ya wanafunzi mbalimbali nchini ambao wamekuwa wakiyatoa kuhusu upendeleo wa utoaji mikopo kwa kupata mikopo kwa wanafunzi wenye sifa huku wale wasiokuwa na sifa stahiki wakikosa mikopo hiyo.

“Kwenye hili tunakaribisha watu watoe taarifa kwa sababu kama kuna mtoto wa Mkenda uliyesoma naye utakuwa unamjua baba yake ni nani na uwezo wake, halafu wewe unaona mtu huyo amepewa mkopo toa taarifa” amesema Waziri Mkenda na kuongeza;

“Mtu yeyote ambaye ana wasiwasi na utoaji wa mikopo tunamkaribisha ili aweze kuisaidia tume kufanya kazi yake kwa kuwa na taarifa zenye usahihi wa hali ya juu kutoka kwa wanachi husika”

Profesa Mkenda amesema kuwa tume hiyo itaangalia vigezo vilivyoainishwa ili kuona kama kuna taarifa zingine za ziada zinaweza kutumika katika utoaji wa mikopo ili fedha zinazotolewa na Serikali zikopeshwe kwa haki.

Waziri Mkenda amewahimiza waombaji mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka 2022/2023 kusoma na kuuzingatia ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa mwaka 2022/2023’ ili kuwasilisha maombi kwa usahihi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi zilizowekwa kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Chanzo: Mwananchi