Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb.) leo tarehe 16 Mei 2024 amewasili nchini China kuanza ziara ya kikazi.
Ziara hii mbali na kudumisha ushirikiano wa kidiplomasia wa kihistoria uliopo baina ya mataifa haya mawili ni muendelezo wa utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ikilenga kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa wakati wa ziara ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoifanya nchini humo Novemba 2 – 4, 2022.
Akiwa China, Waziri Makamba anatarajia kufanya mazungumzo na mwenyeji wake Mhe. WANG Yi ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa China.
Miongoni mwa masuala muhimu yanayotarajiwa kujadiliwa kwenye ziara hii ni pamoja na maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) unaotekelezwa na kampuni ya CCECC, maboresho ya reli ya TAZARA na uwekezaji kwenye mradi wa uchimbaji wa chuma wa Liganga na Mchuchuma.
Aidha Waziri Makamba na mwenyeji wake wanatarajia kujadili masula mbalimbali muhimu ya ushirikiano baina ya China na Afrika yanayoratibiwa kupitia Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama, kuelekea Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwa hilo unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu 2024.
Vilevile Makamba atafanya mazungumzo na viongozi wengine waandamizi wa Serikali na wakuu wa mashirika ya kimkakati wakiwemo Rais wa Shirika la Ushikiano wa Maendeleo ya Kimataifa (CIDCA), Rais wa Benki ya EXIM ya China na kampuni ya HUAWEI.
Kadhalika, Waziri Makamba atafanya mazungumzo na Mabalozi wa Nchi Wanachama wa SADC wanaziwakilisha nchi zao nchini China.
Mwaka huu, Tanzania na China zimetimiza miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia ulioanzishwa na waasisi wa mataifa hayo mawili, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Mao Zedong.