Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Nuru Mhando na Meneja wa Matumizi ya Fedha wa TPA, Witness Mahela ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazowakabili.
Majaliwa amefikia uamuzu huo leo jijini Dar es Salaam katika kikao chake na Waziri na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Menejimenti ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU na Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) kilichofanyika katika ofisi za TPA.
Majaliwa amechukua hatua hiyo baada kupokea ripoti ya Ukaguzi Maalum uliofanywa na CAG katika hesabu ya Bandari ya Kigoma kwa mwaka 2017/2018 na 2018/2019, iliyokuwa na lengo kujiridhisha kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma katika taasisi hiyo.
Aidha, amemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya ukaguzi maalum kwenye bandari za Dar es Salaam, Mwanza, Mtwara, Tanga na Kyela kutokana na kuwepo wa matumizi mabaya ya fedha za umma katika bandari hizo.