Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wazazi wa mhitimu SUA aliyeuawa wamwangukia Rais Samia

Video Archive
Thu, 23 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vilio na simanzi vimetawala katika mazishi ya mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Magreth Mashuwe (22), huku wazazi wake wakimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mauaji hayo ya kinyama ili wale waliohusika wachukuliwe hatua.

Mazishi hayo yamefanyika leo Alhamisi Desemba 23 kwenye makaburi ya familia katika kijiji cha Shimbi Kati, wilayani hapa mkoani Kilimanjaro.

Mashuwe aliuawa Desemba 14 na mwili wake kutupwa katika shamba la chuo hicho.

Tayari Jeshi la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia mwanaume mmoja anayedaiwa kuwa mchumba wa Magreth kuhusiana na mauaji hayo.

Akizungumza huku akibubujikwa na machozi, mama mzazi wa Magreth, Petronila Temu amesema kifo cha mwanaye ni pigo kubwa kwao, huku akimwomba Rais Samia kubeba maumivu yao na kuhakikisha wale wote waliokatisha uhai mtoto wao wanakamatwa na kuchukuliwa hatua.

"Mama Samia ni mwanamke mwenzangu, naomba usikie kilio changu huko uliko mama, unisaidie ili hawa waliomuua mwanangu ambaye hana hatia waweze kukamatwa na kuchukuliwa hatua, nisaidie mama Samia," amesema mama huyo huku akitokwa na machozi.

Naye baba mzazi wa Magreth, Liberat Mashuwe, ameeleza kwa masikitiko makubwa namna alivyowekeza nguvu kubwa kwenye elimu ya mwanaye ili baadaye awe msaada kwa familia.

"Maumivu niliyonayo Mungu ndiye anayeweza kujua, naiomba serikali ambayo ninaiamini itusaidie kuwapata hawa wauaji wa mwanangu.

“Mwanangu alikuwa ni tegemeo kubwa kwa familia nami nilipambana kuhakikisha anafikia malengo yake lakini baada ya kumaliza chuo wauaji wamekatisha uhai wake," amesema baba wa Magreth.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live