Watahiniwa 1,230,780 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya Msingi(PSLE) kesho Jumatano Septemba 11, 2024 huku Baraza la Mtihani Tanzania(NECTA) likiwatahadharisha kuwafutia matokeo watakaobanika kufanya udanganyifu.
Mtihani huo unatarajiwa kufanyika kwa siku mbili, utaanza kesho na kuhitimishwa Septemba 12, 2024.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Septemba 10, 2024 na Katibu mtendaji wa baraza hilo, Said Mohamed alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo.
Mohamed amesema katika watahiniwa hao, 564,176 sawa na asilimia 45.84 ni wasichana na wavulana ni 666,604 sawa na asilimia 54.16.
Amesema watahiniwa wenye mahitaji maalumu waliosailiwa kufanya mtihani huo ni 4,583 kati yao 98 ni wasioona,1402 wenye uoni hafifu,1067 wenye uziwi, 486 wenye ulemavu wa akili na 1530 ni wenye ulemavu wa viungo.
“Kati ya watahiniwa 1,230,780 waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka 2024, watahiniwa 1,158,862 sawa na asilimia 94.16 watafanya mtihani wa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 sawa na asilimia 5.84 watafanya mtihani wa lugha ya kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,"amesema katibu huyo.
Kuhusu masomo watakayotahiniwa, amesema ni sita ambayo ni Kiswahili, lugha ya kingereza, sayansi na teknolojia, hisabati, maarifa ya jamii, stadi za maisha na uraia.
Akielezea kuhusu maandalizi, Mohamed amesema yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo katoka halmashauri na manispaa zote nchini.