Rais Samia Suluhu Hassan, amewaonya watu wote ambao wanaodhani kwamba Hayati Dk. John Pombe Magufuli ameondoka na mipango yake ya usimamizi wa mali za umma, kupambana na ukwepaji kodi, kuziba mianya ya kupoteza mapato, kukemea uzembe na wizi na kusisitiza kwamba serikali yake itaendelea na mipango hiyo kama alivyoianzisha Hayati Magufuli.
Rais Samia ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma, wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kueleza dira ya serikali yake, katika kuwaletea wananchi maendeleo ambapo amesisitiza kwamba serikali yake haitarudishwa nyuma katika mapambazo dhidi ya watu wanaochezea rasilimali za nchi.
“Ninajua watakuwepo baadhi ya watu wenye wasiwasi kutokana na jinsia yangu kwamba sitaweza kutekeleza yote niliyoyasema, ningependa kuwaondoa hofu kwani Mwenyezi Mungu hakuumba ubongo hafifu kwa mwanamke na ubongo makini kwa mwanaume wote tulizaliwa sawa.
“Ninataka niwahakikishie kwamba nimekuzwa kwenye jamii sahihi na nina uzoefu wa kutosha kwenye shughuli za serikali na kwenye chama changu hivyo ninaamini kwamba ninao uwezo wa kuliongoza taifa langu,” Rais Samia Suluhu
Pia Rais Samia amekemea vikali watu wanaotumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za uchonganishi kuhusu kifo cha Hayati Magufuli wakidai alipewa sumu au kuwekewa vitu vilivyosababisha kifo chake na kuwataka waache mara moja vinginevyo sheria itachukua mkondo wake.
“Wanaosema mitandaoni kuwa Hayati Magufuli alipewa sumu, mara fulani na fulani walitega kitu, ni za kugonganisha Koo na Koo, Makabila na Makabila, wanaochanganisha, kama wana taarifa za maana waje tuwasikilize, vyombo vya upelelezi vipo vitafanya kazi yake, la sivyo waache kuleta uchonganishi, kama wanafanya hivyo wakidhani hatutowapata, warudi kwa Mungu wajiulize je wanafanya sawa?”
Mambo mengine yaliyozungumwa na Rais Samia katika hotuba yake hiyo iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wastaafu, ni pamoja na serikali kurudisha imani kwa wawekezaji na kujenga mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje, ikiwa ni pamoja na kuunda sera nzuri, kusimamia ulipaji rafiki wa na kupunguza urasimu serikalini.
Pia ameeleza kwamba serikali itaanzisha mchakato wa kuyapitia mashirika ya umma ili yaweze kujiendesha kwa faida, serikali itakutana na wadau wa sekta binafsi na kuangalia namna ya kufanya nao kazi kwa tija ikiwa ni pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini.
Pia amesema serikali ipo kwenye mpango wa kuhakikisha inalilea shirika la ndege ATCL kimkakati kwa kufanya uchambuzi wa kina kuhakikisha shirika hilo linajiendesha kwa faida.