Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanandoa, 'house boy' wafikisha siku 205 mahabusu, upelelezi bado

Ndoa2 Mmn Mshtakiwa Najim Mohamed (52) akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Mon, 22 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mshtakiwa katika kesi ya kusafirisha kilo 3,050 za dawa za kulevya, Najim Mohamed (52) na mkewe Maryam Mohamedi (50) pamoja na  mfanyakazi wa ndani, Juma Abbas (37), wamefikisha siku 205 wakiwa mahabusu bila upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Washtakiwa hao wanaendelea kusota mahabusu kutokana na mashtaka yanayowakabili ya kusafirisha dawa za kulevya kutokuwa na dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mohamed na wenzake anakabiliwa na kesi ya uhujumu yenye mashtaka mawili ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini na Methamphetamine.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Desemba 29, 2023 na kusomewa kesi hiyo.

Hata hivyo, tangu siku hiyo hadi leo Julai 22, 2024, kesi hiyo ilipotajwa, washtakiwa wamefikishwa siku 205 wakiwa mahabusu kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokukamilika.

Awali, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, Wakili Frank Rimoy aliieleza Mahakama kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Lyamuya alikubali ombi hilo na kuahirisha kesi hadi Agosti 5, 2024 itakapotajwa. Kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video, huku washtakiwa wakiwa rumande.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa  Desemba 15, 2023 katika eneo la Kibugumo Shule lililopo Wilaya ya Kigamboni, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroini zenye uzito wa kilo 882.71.

Shtaka la pili, wanadaiwa siku hiyoo walisafirisha dawa za kulevya aina ya Methamphetamine zenye uzito wa kilo 2167.29.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live