Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waliofariki kwa maporomoko Same wafikia watatu

Maporomoko DRC Amauti.png Maporomoko

Sat, 13 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Idadi ya watu waliofariki dunia kufuatia maporomoko ya udongo wilayani Same, Mkoa wa Kilimanjaro imeongezeka na kufikia watu watatu.

 Maporomoko hayo yanasababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha milimani wilayani humo.

Januari 10, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alithibitisha kutokea kwa vifo vya watu wawili akiwemo mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Lugulu, Ramadhan Ayoub Mduma (12) na Noel Gilbert (17) waliofariki baada ya nyumba walizokuwa wamelala kuangukiwa na maporomoko hayo.

Hata hivyo, akizungumza jana Januari 11, 2024 mkuu wa wilaya hiyo, Kasilda Mgeni amesema vifo vimeongezeka na kufikia watu watatu baada ya mwili mwanaume, Stephen Samson (54), mkazi wa Bwambo kukutwa umekwama kwenye mawe ndani ya mto.

"Idadi ya vifo vimefikia vitatu, baada ya mtu mmoja mkazi wa Bwambo mwili wake kukutwa umekwama kwenye mawe ndani ya mto, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na tayari umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za maziko," amesema DC Kasilda.

Maporomoko ya mawe na udongo ambayo yameziba baadhi ya barabara na kusababisha kukatika kwa mawasiliano wilayani humo hasa maeneo ya milimani yamesababisha adha kubwa ikiwemo watu kushindwa kusafiri kutoka maeneo ya milimani kuja tambarare.

Mgeni amesema mpaka sasa kilometa zaidi ya 80 za barabara kwenye maeneo yalikombumbwa na maporomoko hayo zimeathiriwa, huku kaya zaidi 15 zikikosa makazi baada ya nyumba zao kuzama kwenye maji.

“Zaidi ya kilomita 80 za barabara zimeathiriwa pamoja na madaraja kadhaa yameharibika kutokana na mafuriko yaliyosababisha barabara kufungwa na kuathiri shughuli za usafiri kusimama kwa muda mrefu katika kata za maeneo ya milimani na ekari 120 za mpunga zimesombwa na maji," amesema.

Amezitaja barabara zilizoathiriwa kuwa ni Kizangaze-Vumba kwenda Mtii ambayo imefungwa na maporomoko ya udongo na barabara ya Ndungu-Lugulu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live