Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Walimu shule za CCM wadai kukosa utulivu

Walimu Pic Walimu shule za CCM wadai kukosa utulivu

Tue, 23 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), umesema licha ya matokeo mazuri ya kidato cha sita mwaka huu, wanakosa utulivu na kutoijua kesho yao kutokana na maelekezo mengi kutoka juu na maisha magumu wanayopitia.

Wakizungumza katika hafla ya kuwapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Ivumwe iliyofanyika usiku wa kuamkia Julai 22, umoja huo umesema licha ya uzalendo ulionao kuweka misingi ya ufaulu, lakini unapitia wakati mgumu kufikia malengo.

Mwenyekiti wa umoja huo, Jacob Msigwa amesema wamekuwa katika wakati mgumu kwa kukosa uhakika wa kubaki kituo cha kazi kutokana na maelekezo mengi, huku maslahi nayo yakiwaumiza.

Amesema mwaka huu wamevunja rekodi katika mtihani wa kidato cha sita, ambapo kati ya wanafunzi 660 kutoka shule sita za jumuiya hiyo mkoani humo, watahiniwa 430 wamepata daraja la kwanza na wengine daraja la pili na tatu.

"Pamoja na mafanikio haya, hatuna uhakika wa kesho, tunatumia uzalendo ila inakatisha tamaa. Hizi ni shule za chama kinachoongoza dola, lakini tunapitia changamoto za miundombinu ya kiutawala" amesema Msigwa.

Mwenyekiti huyo ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sangu ameongeza kuwa ushindi wa chama unategemea zaidi matokeo mazuri ya shule hizo, akieleza kuwa idadi kubwa ya wanafunzi inatokana na juhudi na uzalendo wa wakuu wa shule.

"Kutokana na mafanikio haya kwa mwaka huu, tunatarajia kuwa na hafla ya kupongezana kwa ujumla mwishoni mwa mwezi huu, lengo ni kuhamasishana na kuthamini kazi ya kila mmoja" amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ivumwe, Oscar Mwaihabi amesema mwaka huu wamekuwa na matokeo mazuri ambayo hayajawahi kupatikana tangu kuanza kwa shule hiyo.

Amesema ufaulu wa daraja la kwanza na la pili pekee umewaongeza ari ya kufanya vizuri na kuahidi mwakani mkakati wao ni kufuta daraja la pili na kubakiwa na la kwanza pekee.

"Katika kuhamasisha mafanikio zaidi, tuna walimu tisa ambao tutawapeleka Zanzibar kwa mapumziko kuanzia Alhamisi ya wiki hii," amesema Mwaihabi.

Akizungumzia changamoto hizo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge amesema atakutana na viongozi wa bodi, wakuu wa shule na jhumuiya za wazazi Alhamisi ya wiki hii kujadili kero zote na kuzipatia ufumbuzi.

Kuhusu kuingiliwa majukumu na maelekezo mengi, Mwalunenge amewataka walimu kufanya kazi na kwamba changamoto zao zitatatuliwa kuanzia sasa.

"Sisi ndio chama chenye Serikali, ikiwezekana tutamualika Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi Taifa aje hapa Mbeya tuzungumze naye, lakini naamini kikao chetu cha Alhamisi tutapata suluhisho," amesema Mwalunenge na kuongeza kuwa malengo yao ni kuona watoto wanashinda ili kukipa hadhi chama na Taifa kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live