Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wabunge wapewa tahadhari sheria ya rushwa ya ngono

Rebecca Gyumi Wabunge wapewa tahadhari sheria ya rushwa ya ngono

Sat, 31 Aug 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ukitarajiwa kuwasilishwa bungeni Septemba 2, 2024, mtandao wa kupinga rushwa ya ngono, umewataka wabunge kutoupitisha wakidai unalenga kuwanyamizisha waathirika na kuwapa nguvu wenye mamlaka wanaofanya vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa mtandao huo, kifungu cha 10(b) ambacho kimeongezwa kwenye mabadiliko ya sheria hiyo, kinalenga kuhalalisha matumizi mabaya ya mamlaka kwa njia ya kumhukumu mwathirika wa rushwa ya ngono kama mbinu ya kuwanyamazisha.

Kifungu hicho kinaeleza mtu yeyote ambaye amemsababishia mwenye mamlaka kufanya kosa kwa kumuahidi, kumshawishi kwa kutoa rushwa ya ngono ili apendelewe, epewe cheo, ajira au kupandishwa cheo anakuwa hatiani kwa kosa la rushwa ya ngono.

Muswada huo unawasilishwa bungeni baada ya kufanyiwa marekebisho kifungu cha 25 cha sheria hiyo kinachozungumzia rushwa ya ngono na kuweka kipengele kinachoeleza, ili kuwapo rushwa lazima awepo mtoaji na mpokeaji.

Akizungumza leo Agosti 31, 2024 kwa niaba ya mtandao huo, mwanaharakati, Rebeca Gyumi amesema endapo wabunge watapitisha mabadiliko hayo watakuwa wamechangia kuiangamiza jamii ambayo imeathiriwa na aina hiyo ya rushwa.

Rebeca amesema tatizo la rushwa ya ngono limeendelea kuota mizizi na sasa athari zake zinaonekana kwa jinsi zote, tofauti na ilivyokuwa awali waathirika wakuu wakiwa wanawake.

“Sasa hivi rushwa ya ngono inakula pande zote, tena mbaya zaidi kwa vijana wa kiume wao wanaombwa rushwa ya ngono na wanawake wenye mamlaka na wakati mwingine wanaume wenzao, endapo tutaruhusu wanaofanya vitendo hivi kupata mwanya wa kutokea tutaangamiza kundi kubwa.

“Kuleta mabadiliko ambayo yanalenga kumshtaki pia anayetoa rushwa hiyo ni wazi kwamba tunataka kuwafunga midomo waathirika kwa kuwa mara nyingi wanaoomba aina hii ya rushwa ni watu wenye mamlaka,” amesema Rebeca.

Akizungumza katika mkutano huo, mwanaharakati mwingine, Dk Ananilea Nkya amesema kama wabunge wataruhusu kupita muswada huo, watakuwa wamejichimbia shimo hata wao wenyewe, hasa kuelekea katika chaguzi zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu na mwakani.

“Tunafahamu kwamba huko kwenye siasa ndiko changamoto. Sasa kama tulipigana kuipata sheria ambayo inawawajibisha waomba rushwa ya ngono halafu leo kinatengenezwa kifungu cha kuwalinda, halafu wabunge wakapitisha mabadiliko hayo ni wazi wataturudisha gizani,” amesema.

Akitoa ushuhuda wake, Dk Ananilea amesema ni miongoni mwa waathirika wa rushwa ya ngono iliyomsababishia kunyimwa fursa ya kwenda nje ya nchi baada ya kushindwa kukidhi matakwa ya bosi wake.

“Nikiwa nafanya kazi kwenye taasisi fulani, kuna watu waliniona na kunipa safari ya kwenda China lakini bosi wangu alikataa kunipa ruhusa kwa sababu nilikataa kujihusisha naye kimapenzi, vitendo kama hivi vinakatisha tamaa na kuangamiza watu wengi, sasa sitaki niliyopitia mimi miaka hiyo yaendelee kuwakuta vijana.

“Tunakosa kuwa na vijana wabunifu kwa sababu huenda nafasi zao zinachukuliwa na wanaolazimishwa kutoa ngono ili watolewe kutoka hatua moja kwenda nyingine. Hatuwezi kuendelea kwa utaratibu huu lazima wanaofanya hivi wawajibishwe kusiwe na namna yoyote ya kuwalinda,” amesema.

Ushuhuda wa aina hiyo umetolewa pia na Asha Omary ambaye amedai aliombwa rushwa ya ngono na daktari aliyekuwa anamtibu bibi yake.

“Daktari alimwandikia bibi yangu dawa za kutumia kila mwezi, sikuwa na uwezo huo akaniambia nikikubali kushiriki naye ngono atawezesha niwe napata dawa hizo, nilikuwa katikati ya kuamua niokoe maisha ya bibi yangu au nilinde utu wangu,” amesema.

Chanzo: Mwanaspoti