Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vyama 10 vya upinzani vyamvaa Jaji Mutungi

Video Archive
Sat, 22 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Vyama 10 vya upinzani nchini Tanzania vimemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kurejesha ratiba za vikao vya Baraza la Vyama vya Siasa ili kupata fursa ya kujadili Muswada wa Marekebisho ya Vyama vya Siasa kabla ya kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge.

Akizungumza leo Jumamosi Desemba 22, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akisoma tamko la vyama hivyo, naibu katibu mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu amesema kikao cha kamati ya uongozi ya baraza kilichoketi Desemba 4, 2018, wajumbe walikubaliana Desemba 21 na 22, 2018 kifanyike kikao kujadili muswada huo.

Vyama hivyo ni ACT-Wazalendo, ADC, CCK, Chaumma, CUF, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi, NLD na UPDP.

Muswada huo umesomwa kwa mara ya kwanza bungeni ambako Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema Spika wa Bunge, Job Ndugai ataipangia Kamati ya Bunge itakayofanya uchambuzi.

Mwalimu amesema kupitia kikao hicho  vyama vya siasa  vingepata fursa ya kuupitia na kujadili muswada husika na kisha kutoa msimamo wa pamoja wa baraza hilo.

Amesema wanashangazwa na uamuzi wa Msajili kwa maelezo kuwa ameahirisha kikao hicho na kukwamisha lengo lao la kujiandaa kutumia fursa hiyo kuzungumzia muswada huo aliodai kuwa ni kandamizi.

Mwalimu amesema Msajili hakushauriana na Kamati ya uongozi ya Baraza na kufikia uamuzi wa kuahirisha kikao hicho.

"Hakushauriana na wala hakukuwepo na kikao cha kamati ya Baraza la uongozi. Uamuzi wa kuahirisha  umefanywa na msajili kwa kushirikiana na watu wake,” amesema Mwalimu.

Kifungu cha 19 kinapendekezwa kurekebishwa ili kumwezesha msajili wa vyama vya siasa kufuta usajili wa chama cha siasa kitakachobainika kuwa kilipata usajili kwa njia zisizo za halali.

Muswada huo unalenga katika kuzuia viongozi wa vyama vya siasa kutokuwa wajumbe wa bodi ya wadhamini.

Muswada pia unapendekeza kufuta kifungu cha 21A na kifungu cha 21B kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuliwezesha Baraza la Vyama vya Siasa kupata fedha kutoka katika bajeti ya Serikali na wafadhili.

Unapendekeza pia kuongezwa kwa vifungu ili kuainisha makosa na adhabu na kusitishwa kwa usajili wa vyama vya siasa vitakavyokiuka masharti ya sheria.

Pia, inapendekeza kufanyiwa marekebisho ili kumpa mamlaka waziri mwenye mamlaka ya kutengeneza kanuni za uandaaji wa taarifa za hesabu za vyama vya siasa na mambo yatakayojumuishwa katika katiba za vyama vya siasa.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz