Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vibanda vyateketea stendi ya Msamvu Morogoro

Motoooo AA4ALI.jpeg Vibanda vyateketea stendi ya Msamvu Morogoro

Wed, 24 Jul 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani humo linafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha moto ulioteketeza vibanda 9 vya wafanyabiashara wadogo waliopo pembezoni mwa Kituo Kikuu cha Mabasi, Msamvu Mjini Morogoro.

Tukio hilo limetokea usiku wa Julai 23, 2024 majira ya saa 3:15 ambapo kumeshuhudiwa moto ulioibuka ghafla na kuteketeza vibanda vya baadhi ya wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa Kituo hicho cha mabasi yaendayo mikoani.

Sababu za moto huo bado zina utata, wengine wakieleza kuwa kulikuwa na moto kwenye moja ya kibanda, wengine wakisema ni hitilafu ya umeme.

Akizungumza mara baada ya zoezi la kuzima moto huo, Ofisa wa Oparesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ASF Daniel Myalla anasema walipokea wito huo mnamo saa 4:01 usiku ambapo walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa mali za vibanda vingine zaidi ya 50 pamoja na kudhibiti moto huo.

"Tulipokea taarifa ya uwepo wa moto katika eneo la stendi ya mabasi Msamvu. Tukafika hapa na magari mawili ya kuzima moto, tulikuta unaunguza vibanda kama nane au tisa, tukavizima ili visije kuharibu vingine.

“Mpaka sasa hatujajua chanzo cha moto huo, lakini tutaendelea kushirikiana na wadau wengine kufanya uchunguzi kubaini chanzo chake na tathmini ya uharibifu," amesema Miala.

"Ukiangalia hapa kuna vibanda kama 60 na kama tusingeudhibiti moto mapema, vingeweza kuungua hata vibanda 50. Tunawashukuru wananchi kwa kutoa taarifa mapema."

Mashuhuda wa tukio la moto huo wamelipongeza jeshi hilo kwa kufika mapema na kusaidia kuzima moto huo. Wamesema huenda chanzo ni moto wa kupikia ambao haukuzimwa vizuri huku wengine wakidai ni hitilafu ya umeme.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa White House, Kata ya Mafisa, Manispaa ya Morogoro mahali kilipo kituo hicho cha mabasi, Saidi Daudi amepongeza jitihada zilizofanywa na Jeshi hilo kwa kuwasili mapema eneo la tukio na kushirikiana na wananchi kuudhibiti moto huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live