Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wiki mbaya kwa wataalamu wa afya, watano wafa ajalini

Video Archive
Sat, 23 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Handeni. Ni wiki mbaya kwa wataalam wa afya. Ndani ya siku mbili, wataalam watano wa sekta ya afya wamefariki katika ajali mbili za barabarani na kuacha pengo kubwa.

Alhamisi usiku wataalamu wa afya watatu wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga walifariki katika ajali baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka saa 4 usiku katika kijiji cha Taula kata ya Kwedizinga.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Handeni, William Makufwe aliwataja watumishi hao kuwa ni Lazaro Zabron, Mussa Muro na Lucas Lubacha waliokuwa wameajiriwa kama madaktari.

Siku moja baada ya ajali hiyo ya Handeni, madaktari wengine waliokuwa wakisafiri kutoka Mbeya kuja Dar es Salaam walikufa kwenye ajali ya barabarani.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwataja watumishi hao kuwa ni Florence Evarist Tairo wa kitengo cha dharura cha wizara hiyo na mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Kachwamba aliyekuwa mtaalamu wa magonjwa ya ngozi.

“Huu ni msiba mzito kwa wanafamilia waliopoteza wapendwa wao, wizara na jamii kwa jumla,’’ alisema Waziri Ummy katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram jana.

William Makufwe, mkurugenzi wa Handeni alisema Lubacha na Muro walikuwa wakifanya kazi katika kituo cha afya Mkata wakati Zabron alikuwa kituo cha afya cha Kabuku.

“Walikuwa wakirudi kutoka kwenye semina mjini Moshi na walichukua basi la Tanga. Walishuka Segera kwenye makutano ya barabara na kuchukua lori lililokuwa likielekea kwenye vituo vya kazi. Lori lilipinduka na ndivyo walivyokufa,” alisema.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alilitaja lori hilo aina ya Volvo lenye namba za usajili T 697 ASN, akisema bado wanachunguza sababu ya lori hilo kupinduka.

“Dereva wa lori hilo yuko mahututi hospitalini, lakini mtoto wake wa kiume pia amefariki,” alisema Bukombe.

Alisema miili miwili ya wataalamu hao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Handeni na mwingine katika Hospitali ya Magunga Korogwe ambako pia dereva Bakari Mohamed (29) akiwa hajitambui kutokana na majeraha makubwa.

Jana miili ya madaktari watatu waliopata ajali wakiwa kwenye lori iliagwa katika viwanja vya kituo cha afya wilayani Handeni, Mkata mkoani Tanga.

Makufwe alisema vifo vya madaktari hao vimeacha pengo na kubainisha kuwa wilaya ya Handeni ina uhaba wa madaktari na watumishi wa sekta hiyo asilimia 75 na asilimia 25 waliokuwepo ni pamoja na madaktari hao watatu waliofariki ajalini.

“Kazi waliyokwenda kuifanya Moshi ilikuwa kupata mafunzo kwa ajili ya mashine ya Utra Sound kwa ufadhili wa wenzetu kutoka Ujerumani ili kuongeza ufanisi katika huduma hizo,” alisema Makufwe.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martin Shigela alimtaka katibu tawala mkoa wa Tanga kuhakikisha wanaletwa madaktari wengine haraka ili kuziba pengo hilo la madaktari.

Alisema nafasi za madaktari hao ni nyeti kutokana na huduma zinazohitajika hivyo ni muhimu kuletwa madaktari wegine haraka.

Chanzo: mwananchi.co.tz