Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Waziri Lukuvi atengua uteuzi wa Mchechu NHC

Video Archive
Thu, 21 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Miezi sita tangu waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alipomsimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, sasa ametengua uteuzi wake.

Waziri Lukuvi alitangaza kutengua uteuzi wa Mchechu kuanzia jana. Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ukumbi wa Idara ya Habari bungeni jijini Dodoma, alisema amefikia uamuzi huo kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 18 (1) cha Sheria ya NHC ya mwaka 1990 na marekebisho ya mwaka 2005 kikisomwa pamoja na kifungu cha 48(1)(a) cha sheria ya kutafsiri sheria sura ya kwanza.

Alipoulizwa na Mwananchi ni kipi wamebaini baada ya kumsimamisha Mchechu hadi kufikia hatua ya kutengua uteuzi wake, Lukuvi alijibu akisema, “Mimi ndiye mwenye mamlaka ya kumteua na mimi ndiye nimetengua.”

Desemba 16 mwaka jana, Waziri Lukuvi alimsimamisha kazi Mchechu aliyeteuliwa kuliongoza shirika hilo Machi Mosi, 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa ofisa mtendaji mkuu wa Benki ya CBA.

Lukuvi alipomsimamisha kazi Mchechu alisema uamuzi huo aliufikia kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.

Desemba 13, wakati Rais John Magufuli akizindua nyumba 300 za shirika hilo alieleza hujuma zinazofanywa na viongozi wa NHC, akiwemo Mchechu na Bodi ya Wakurugenzi. “Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako. Unanunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandikia kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako, mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya,” alisema Rais.

Katika hotuba yake, Rais alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi kwa maelezo kuwa wapo wanaotaka nafasi yake na kutumia wajumbe wa bodi na wanasiasa kumchafua.

“Wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu,” alisema Rais Magufuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz