Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Wanafunzi 13 wazuiwa kuendelea darasa la saba kwa kutofanya mtihani darasa la nne

Video Archive
Fri, 27 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita. Wanafunzi 13 wa darasa la sita Shule ya Msingi Ludete wilayani Geita nchini Tanzania hawajui hatma yao ya kumaliza elimu ya msingi baada ya majina yao kutoonekana katika orodha ya wanafunzi wanaopaswa kuingia darasa la saba mwaka 2020.

Wakizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Septemba 26, 2019 wanafunzi hao waliokuwa wameambatana na wazazi wao wamesema licha ya kuwa wanahudhuria darasani na kufanya mitihani na majaribio, wameelezwa hawana sifa za kuingia darasa la saba kwa kuwa walifeli mitihani ya darasa la nne mwaka 2017.

Simon Shija (13),  amesema hakuwahi kuelezwa kama alifeli mtihani wa darasa la nne na amekua akihudhuria shuleni bila shida lakini baada ya likizo ya mwezi Septemba, haitwi jina na alipouliza alielezwa jina lake halipo miongoni mwa wanafunzi watakaoingia darasa la saba mwakani

“Nilifanya mtihani mwaka 2017 na nikaingia darasa la tano sikuambiwa kama nimefeli sasa mwalimu ananiambia nirudie darasa la nne kama ninataka kumaliza la saba, naona bora nibaki mtaani kuliko kuanza tena darasa la nne wadogo zangu wananipita siwezi" amesema Simon.

Baadhi ya wazazi wamesema kitendo cha kuwarudisha watoto darasa la nne ni uonevu na kuwakatisha tamaa na kuhoji kwa nini walimu wamefanya siri kwa miaka miwili huku watoto wakiendelea na masomo ya darasa la tano na sita.

John Charles, mmoja wa wazazi wa wanafunzi hao amemuomba Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako kuingilia kati jambo hilo ili wanafunzi hao watendewe haki kwa uzembe uliofanywa na walimu.

Pia Soma

Advertisement
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Geita, Ali Kidwaka amekiri wanafunzi hao kusoma miaka miwili kimakosa na kusema jambo hilo limesababishwa na uzembe wa mwalimu mkuu pamoja na walimu.

Kidwaka ametoa siku tatu kwa ofisa elimu msingi wa halmashauri hiyo kuchunguza jambo hilo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa waliosababisha watoto kusoma miaka miwili wakiwa hawana sifa.

Hata hivyo, amewataka watoto hao kurudia darasa la nne ili waweze kufanya mitihani ambayo itawapa sifa ya kuendelea hadi darasa la saba.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz