Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Viongozi 1,780 wa CCM wahudhuria mkutano ulioitishwa na Magufuli

Video Archive
Fri, 24 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema mkutano wa chama hicho tawala ulioitishwa na Rais John Magufuli  umehudhuriwa na wajumbe 1,780 kati ya 1,800 waliotakiwa kuwepo.

Dk Bashiru ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Walioshiriki mkutano huo ni viongozi wa CCM ngazi ya mikoa na wilaya kutoka Mikoa yote nchini.

Amesema wajumbe 20 wameshindwa kuhudhuria mkutano huo kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya.

“Ulinipa maelekezo (Magufuli-mwenyekiti wa CCM) ya kuitisha mkutano huu na wajumbe 1,780 wamehudhuria kati ya wajumbe 1,800 waliotakiwa kuwepo," amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Dk Bashiru amesema chama hicho kinajiandaa kuadhimisha miaka 43 tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu itakuwa, Tumeahidi, tumetekeleza.

Pia Soma

Advertisement
Amesema chama hicho pia kinaandaa Ilani ya uchaguzi mkuu wa 2020 na kwamba makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ndiyo mwenyekiti wa kamati hiyo.

Amesema makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ni makamu wa kamati hiyo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni mjumbe.

Amemhakikishia mwenyekiti wa chama hicho kwamba CCM iko imara na imejiandaa kushinda uchaguzi wa mwaka 2020 kutokana na utendaji mzuri wa viongozi wake wa ngazi mbalimbali.

Takribani wiki moja iliyopita zilisambaa taarifa za Rais Magufuli kuwaita viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam, kuzua mjadala kwenye baadhi ya mitandao ya jamii, huku baadhi ya viongozi wa CCM waliotafutwa kwa simu wakithibitisha kualikwa kuhudhuria mkutano huo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM waliopatikana walisita kuthibitisha kuwepo kwa mkutano huo, ambapo licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kutumiwa barua hiyo kwa njia ya mtandao baada ya kuiomba lakini hakujibu chochote.

Naye Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alipotafutwa kwa simu, alisema hana taarifa kwa kuwa yuko safarini, huku akimtaka mwandishi kuandika kama alivyoona kwenye mitandao ya jamii.

Barua iliyosambaa katika baadhi ya mitandao ya jamii  ilisema Januari 24, 2020 Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama hicho wa mikoa, wilaya na jumuiya zake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Licha ya barua hiyo iliyotolewa na Torry Mkama ambaye ni katibu myeka wa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, ikionyesha kutolewa Januari 17, 2019 katika maelezo yake imeonyesha wajumbe wote watakaoshiriki mkutano huo wanatakiwa kuwasili jijini humo Januari 23, 2020.

Ila leo badala ya mkutano huo kufanyika Ikulu kama ilivyokuwa imeelezwa katika taarifa hiyo, umefanyika katika ukumbi wa JNICC.

Chanzo: mwananchi.co.tz