Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Twaweza waijibu Costech, wagoma kueleza undani

Video Archive
Thu, 19 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Twaweza imejibu kimya kimya barua waliyoandikiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Julai 11. 

Twaweza imechukua hatua hiyo ikiwa ni siku saba baada ya kutakiwa na Costech kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kutoa matokeo ya utafiti bila ruhusa.

Julai 11, Costech iliiandikia barua Twaweza na kuitaka kutoa maelezo hayo ikiwa ni siku chache baada ya kutoa ripoti ya utafiti uliopewa jina la ‘Sauti za Wananchi.’

Matokeo ya utafiti huo yalionyesha kuporomoka kwa ukaribu wa wananchi na vyama vya siasa, utekelezaji wa majukumu kwa viongozi walioko madarakani, Rais anavyotekeleza majukumu tangu alipoingia madarakani na uhuru wa kujieleza katika baadhi ya maeneo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema jana kuwa, barua hiyo imejibiwa tangu Julai 13 na sasa wanasubiri majibu ya Costech. Hata hivyo, Eyakuze hakutaka kuingia kwa undani kuhusu barua hiyo waliyoijibu.

Soma zaidi:

Twaweza yasema haihusiki kusambaza barua ya Costech mitandaoni

Akizungumza na gazeti hili, kaimu mkurugenzi mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alithibitisha Twaweza kujibu barua waliyowaandikia. Hata hivyo hakutaka kuelezea kwa kina kuhusu majibu yaliyotolewa.

Dk Nungu alisema barua hiyo ni ya kiofisi hivyo taratibu za kiofisi zitafuata huku wakihakikisha mawasiliano yao hayatoki nje.

“Hii ni barua ya kiofisi tungependa ibaki ya kiofisi. Hata ile ya mara ya kwanza ilitokea bahati mbaya ikasambazwa mitandaoni sasa tusingependa hayo yajirudie.

“Ninachoweza kusema wamejibu barua yetu kama tulivyowaelekeza ila hatua inayofuata ni taratibu za kiofisi na mawasiliano ya kiofisi yanaendelea,” alisema Dk Nungu.

Barua hiyo ya Costech iliyosambaa mitandaoni ilieleza kuwa Twaweza waliomba kibali cha tafiti nne ambazo mmoja umekamilika na nyingine tatu bado zinaendelea.

Kwa mujibu wa barua hiyo tume hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kusajili na kutoa kibali cha tafiti zote za muda mfupi na mrefu zinazofanywa nchini. “Kwa mujibu wa kifungu cha sheria namba 7 cha mwaka 1986, tume hiyo ndiyo yenye mamlaka kusajili na kutoa kibali cha kufanyika tafiti nchini,” ilisema barua hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz