Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Tatizo si ACT ni mimi-Seif

Video Archive
Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kada mpya wa ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hatua zinazochukuliwa dhidi ya chama hicho zinamlenga yeye binafsi lakini kwa kuwa yuko hai hatakubali kunyamazishwa.

Hata hivyo, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema madai ya Maalim Seif haina ukweli kwani mwaka jana ofisi yake iliipa ACT Wazalendo adhabu ya kusitishiwa ruzuku kwa kutowasilisha hesabu zake na Maalim Seif alikuwa hajaingia ACT.

Alisema hawana shida na Maalim Seif hata kidogo huku akisisitiza kuwa kila chama lazima kizingatie sheria.

Jana, akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Maalim Seif alisema kuna watu wana chuki naye na wala si ACT-Wazalendo ambayo ilikuwapo, lakini haijawahi kufanyiwa inayofanyiwa sasa.

Maalim Seif alikuwa anarejea hatua ya hivi karibuni ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kukiandikia barua chama hicho akieleza nia ya kukifuta.

Pia, alizungumzia hatua ya polisi kuzuia mkutano wake wa ndani na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kupiga marufuku ziara ya chama hicho Zanzibar, ingawa ilikuwa imemalizika.

Related Content

Kiongozi huyo wa zamani wa CUF, alisema kuna watu wana woga naye na wengine wana “personal vendette (chuki binafsi).

Alifafanua kuwa aliwahi kuzungumza na viongozi wawili wakubwa wakamweleza kwamba kuna watu wanamwogopa, wanahofia atavunja Muungano.

“Aliponiambia nitavunja Muungano nikacheka sana. Nikamweleza mimi ninawezaje kuuvunja? Nikasema hata ningekuwa Rais wa Zanzibar nisingeweza kuvunja Muungano, sina jeshi, sina polisi wala usalama wa taifa...” alisema.

Seif aliyewahi pia kuwa waziri kiongozi na baadaye makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar, alisema katika kutaka kumnyamazisha ulipandikizwa mgogoro CUF ili kumwondoa.

Alisema baada ya kesi hiyo kumpa haki Profesa ibrahim Lipumba, hawakuona haja ya kukata rufaa kwa kuwa ingekuwa ni kupoteza muda na pengine kesi ingesikilizwa mwakani wakati uchaguzi umefika.

“Na sisi ni vichwa, tukakaa na kuamua kuwaachia chama,” alisema.

Mwanasiasa huyo alisema hata barua ya msajili kutishia kuifuta ACT-Wazalendo imeibua suala la miaka mitano nyuma na kupenyeza jingine tete la kidini ambalo kwa busara halikupaswa kuibuliwa.

Katika barua hiyo ya Machi 25, Msajili alidai “wafuasi wanaodhaniwa wa Maalim Seif walitumia neno Takbir wakati wanapandisha bendera ya ACT-wazalendo.”

Alipoulizwa kama anadhani kuna mpango wa kufuta chama hicho, alisema uwezekano huo upo kwa kuwa yameshafanyika mambo mengi.

“Hatuwezi kusema (Msajili) hawezi kuifuta ACT. Akiifuta tutajua la kufanya. Wasidhani watamnyamazisha Seif, maadam niko hai sitokubali kunyamazishwa,” alisema.

Tuhuma za wafuasi wake

Akizungumzia madai kuwa wafuasi wake wamechoma bendera na kubadili ofisi za CUF, Maalim alisema hawakufanya fujo zozote, bali baada ya mkutano mkuu kumfukuza yeye na viongozi wengine, baadhi ya wafuasi waliungana nao kutafuta jukwaa jingine la kisiasa.

Alisema majengo mengi yaliyokuwa yanatumiwa na CUF Zanzibar, isipokuwa ofisi mbili za Mtendeni na Kilimahewa ni mali ya watu binafsi na kama wameamua kuhama chama, hawakuwa na sababu ya kubakiza alama wala nembo za CUF.

Kuhusu samani za ofisi hizo, alisema hakukuwa na samani ambazo ni mali za CUF. Mfano ni katika ofisi yangu, kila kilichokuwamo ni mali yangu binafsi,” alisema huku akisisitiza kuwa hata ruzuku ilikuwa inatolewa kwa upande wa Profesa Lipumba kwa miaka zaidi ya miwili.

“Nilimwandikia CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kwamba hakuna fedha za ruzuku ninazopata kwa hiyo sihusiki na zo kwa lolote” alisema.

Licha ya kwamba alikuwa katibu mkuu wa CUF, alisema hakupata fursa ya kukabidhi ofisi kwa kuwa wafuasi wa Lipumba walivamia ofisi ya Buguruni na tangu hapo hakuwahi kufika tena hadi alipofukuzwa.

Aliwashauri Watanzania waendelee kuwa na imani na mahakama kwa kuwa huko ndiko matumaini yaliko.



Chanzo: mwananchi.co.tz