Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Tanzania hakuna ugonjwa wa Ebola

Video Archive
Mon, 16 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema hakuna mtu aliyethibitika kuwa na ugonjwa wa Ebola nchini humo, na watu wawili waliotiliwa shaka na kupimwa imethibitika kuwa hawana maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Septemba 14, 2019 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akiwa na naibu wake, Dk Faustine Ndugulile, mganga mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi na jopo la wataalam  wa Shirika la Afya Duniani (WHO), amewataka wananchi kutokuwa na hofu yoyote.

Amebainisha kuwa taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo nchini zimetokana na watu wawili kudhaniwa kuwa na maambukizi ya Ebola katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.

“Hawa walikuwa wahisiwa lakini wizara imefanya vipimo vya maabara zaidi ya mara moja kama inavyoelekezwa na mwongozo wa WHO na kujiridhisha kwamba hawakuwa  na maambukizi ya virusi vya ebola hivyo hakuna ugonjwa huo Tanzania,” amesema Waziri Ummy.

Amesema Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiandaa ikiwa itatokea waathirika wa ugonjwa huo nchini na kwamba wamejenga vituo vya kutenga watakaotiliwa shaka au kuwa na ugonjwa huo mkoani  Mwanza, Dar es Salaam na Moshi.

Ebola ni nini

Pia Soma

Advertisement

Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na kirusi kiitwacho ebola. Kirusi hicho ni moja kati ya familia ya virusi watatu toka katika familia ya filoviridiae.

Zipo aina tano za kirusi cha ebola ambao nao ni bundibugyo ebolavirus (BDBV), zaire ebolavirus (EBOV), reston ebolavirus (RESTV), sudan ebolavirus (SUDV) na tai forest ebolavirus (TAFV).

Aina hizo tatu za virusi, yaani BDBV, EBOV na RESTV, ndiyo inayongoza kwa kusababisha mlipuko wa ugonjwa huo barani Afrika. Wengine wanapatikana nchi za Asia, yaani Ufilipino na Thailand na mpaka sasa hakuna taarifa za kusababisha vifo.

Kwa mara ya kwanza ugonjwa huu uliripotiwa kutokea mwaka 1976 katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hatari ya mgojwa kupoteza maisha ni asilimia 90. Watu ambao wako katika hatari ya kupata ugonjwa huo ni jamii inayoishi karibu na jamii ya wanyama au watu walioathirika.

Pia uwepo katika mazishi ya wagonjwa wa ebola wakati wa shughuli za kuzika na kugusana na majimaji ya mgonjwa aliyekufa.

Unavyoambukizwa na kuenea

Chanzo cha ugonjwa katika makundi yetu ni mtu mmojawapo kugusana na damu au majimaji ya wanyama walioambukizwa, ambao mara nyingi ni nyani, sokwe, tumbili na popo. Inaaminika kuwa popo wanaopenda kula matunda, wanaeneza ugonjwa huo bila wao kuathirika.

Katika jamii yetu ugonjwa huu huweza kuambukizwa kutoka mtu mmoja mwenye maambukizi kwenda kwa mwingine baada ya kugusana na damu au maji maji kupitia michubuko au majeraha juu ya ngozi.

Watu walio na maambukizi na wakapata nafuu bado wanaweza kuwaambukiza wengine kwa zaidi ya miezi miwili, pia wanaweza kuwaambukiza watu wengine kwa njia ya kujamiana.

Dalili za ugonjwa

Jina jingine la ugonjwa huu ni ‘ugonjwa wa kuvuja damu’. Hii ilitokana kujitokeza dalili ya kuvuja damu mwilini.

Dalili za ugonjwa huu  huanza kujitokeza kuanzia wiki ya pili au ya tatu tangu kugusana na damu au majimaji ya mwilini ya mgonjwa wa ebola.

Dalili zake ni homa kali, maumivu ya koo na misuli, kichwa kuumwa na mwili kuwa dhaifu.

Baadaye dalili zingine hujitokeza baada ya ini na figo kuanza kuathirika dalili hizo ni kama kuhisi kichefu chefu, kutapika na kuharisha.

Uchunguzi na matibabu

Sampuli ya damu ya mgonjwa hupimwa ili kutambua askari mwili maalumu walizalishwa na mwili kupambana dhidi ya virusi ebola. Pia kutazama uwepo wa DNA ya virusi wenyewe.

Ugonjwa huu hauna tiba wala chanjo kama ilivyo kwa magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi ambayo huwa hayana dawa wala chanjo, bali ni matibabu ya kumsaidia mgonjwa kupata ahueni ambayo ni kama vile kuongezewa maji kwa njia ya mshipa.

Mpaka sasa hakuna kampuni wala hospitali iliyopewa leseni ya kuuza au kutengeza chanjo.

Kujikinga na kuudhibiti ugonjwa wa ebola

Ugonjwa huu unaweza kuzuia kujitokeza na kupunguza kuenea kwa kuwachunguza wanyama walio na ugonjwa na kuwaua na kisha kuyatupa mabaki yao.

Kuhakikisha nyama zinapikwa vizuri, kuvaa mavazi maalumu ya kujikinga kwa wale wanaofanya shughuli za wanyama pamoja na watoa huduma za afya.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz