Dar es Salaam. Mgonjwa anayeishi kwa kutegemea mashine ya kumsaidia kupumua (Oxygen Concentrator) Hamad Awadh amepokea msaada wa fedha na kuwezeshwa huduma ya umeme bure na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Awadh (28) amekabidhiwa msaada huo leo Alhamisi Septemba 5, 2019 baada ya Gazeti la Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kuchapisha habari zake jana Jumatano.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo mbele ya vyombo vya habari, Kaimu Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Leila Mhaji amesema fedha hizo zinajumuisha Sh1.5 milioni kwa ajili ya unit za umeme kwa miezi sita na Sh10 milioni kwa ajili ya mchango wa fedha za matibabu nje ya nchi.
“Tumefuatilia katika vyombo vya habari jana kuhusu taarifa za Awadh, uongozi wa Tanesco umeona ni vema ukamsaidia kwa kuwa tunatoa huduma kwa ajili ya jamii, hivyo lazima turudishe pia,” amesema Mhaji.
Meneja wa Tanesco mkoa wa Ilala, Sotco Nombo amesema shirika hilo litamfungia Awadh luku maalum ya peke yake itakayowekwa unit za umeme zenye thamani ya Sh1.5 milioni.
“Gharama za ufungaji umeme zitafanyika kesho chini ya mafundi wa Tanesco na hili lazima mwenye nyumba aliridhie kwanza na gharama zote za ufundi na vifaa zitakuwa chini yetu,” amesema Nombo.