Dar/Mikoani. Ni dhahiri kuwa familia za Asteria Chilambo, Clara Mbalase, Amour Ally na Bernad Mwingizi wiki hii zimetawaliwa na furaha iliyopita kiasi.
Vijana hao wanne ni miongoni mwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa juzi na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).
Asteria, ameshika nafasi ya sita kwa wasichana waliofanya vizuri katika masomo ya sayansi huku Clara akishika nafasi ya tisa na Amour ameshika nafasi ya nne katika wanafunzi kumi waliofanya vizuri kwa ujumla kitaifa.
Akitangaza matokeo hayo mjini Unguja, katibu mtendaji wa Neta, Dk Charles Msonde alisema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.52 baada ya watahiniwa 83,581 kufaulu. Hiyo ni sawa na asilimia 97.58. Mwaka 2017, watahiniwa waliofaulu walikuwa asilimia 70, 552 (sawa na asilimia 96.06).
Mwananchi limefanya mazungumzo na wanafunzi hao ambao wameeleza siri ya mafanikio katika mtihani huo.
Asteria aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Canosa jijini Dar es Salaam unaweza kumuita mtaalamu wa hesabu na hii si mara yake ya kwanza kung’ara kwani aliwahi kuwa miongoni mwa wanafunzi 10 bora katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2016.
Asteria amepata daraja la kwanza katika mchepuo wa PCM. Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita Fizikia amepata B, Kemia (A) na Hesabu (A).
Msichana huyo anasema siri yake ya kuwa mtaalamu wa hesabu ni kuzifanyia mazoezi kila siku.
“Kila somo lina ujanja wake wa kusoma, hesabu hatusomi bali tunazifanyia kazi. Kila siku unavyoikumbusha akili inakumbuka kesho hizi ndiyo hesabu, asubuhi mchana na jioni vitu gani ambavyo mwalimu amefundisha, unavirudia mara kwa mara,” anasema Asteria.
Pamoja na kusoma kwa bidii, anasema alipata mshtuko baada ya kupokea matokeo hayo.
Asteria ambaye kwa sasa anafanya kazi ya kujitolea Masaki jijini Dar es Salaam, anasema alikuwa akiangalia kila mara mtandaoni kama matokeo yametoka.
“Nilipoyaona juzi saa sita, nilifurahi sana nikampigia mama yangu. Nilitarajia kufaulu ila sikutarajia kuwepo 10 bora ya wanawake,” anasema.
Binti huyo mwenye ndoto za kuwa mhandisi anataja siri nyingine ya mafanikio yake kuwa kumtegemea na kumuomba Mungu.
“Siri ya mafanikio ni Mungu kwa sababu kufaulu wengi walikuwa wanasoma kama mimi, ila Mungu. Pia walimu wangu walikuwa wananifuata na kunipatia motisha, walikuwa wananifundisha nifanye nini katika kusoma,” anasema.
Anasema kingine ni kusoma vitabu kwa wingi na majadiliano na wanafunzi wenzake.
“Mama yangu amekuwa rafiki yangu sana, hakuwa akinifokea bali alinielekeza na nimeweza kufanya vyema kupitia yeye,” anasema.
Kwa upande wake, Clara aliyekuwa akisoma Sekondari ya Canosa alipata daraja la kwanza katika mchepuo wa sayansi akichukua Fizikia, Kemia na Hesabu na kushika nafasi ya tisa kitaifa.
Anasema siri ya mafanikio yake imechangiwa na kumuomba Mungu, juhudi binafsi, kujisomea, majadiliano na walimu waliokuwa marafiki wa wanafunzi kitaaluma.
Clara anasema walimu wao wamekuwa wakionyesha mchango mkubwa kwa kuwapa mitihani mingi na kuwaongoza vyema kitaaluma.
“Vitabu ni vingi, tuna maktaba za kutosha, unaingia muda wowote na walimu wanaweza kushinda hapa muda wote kutusaidia,” anasema.
Clara ambaye ni mtoto wa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Gideon Mbalase anasema alipokea matokeo hayo akiwa nyumbani kupitia kwa rafiki zake aliosoma nao.
Anasema mafanikio hayo yamechangiwa na familia yake.
Clara anasema malengo yake ni kuja kuwa mhandisi kwa kuwa ndiyo fani ya kitaaluma anayoipenda.
“Malengo yangu ni kuendelea chuo kikuu nikasomee masomo ya uhandisi wa ujenzi na najua nitaweza, nataka nikapambane na wanaume waone nasi tunaweza,” anasema.
Naye Bernad Mwinginzi wa Shule ya Sekondari Nyarubanda iliyopo mkoani Kigoma ambaye ni miongoni mwa waliofanya vizuri katika masomo ya lugha na sanaa, anasema alistahili kufaulu.
“Kwa nilivyojiandaa vizuri, haya matokeo nilistahili kuyapata. Nadhani ndoto yangu ya kuwa mwandishi wa habari mkubwa sasa itatimia,” anasema Mwingizi.
Anawataka wanafunzi kusoma kwa bidii bila kujali changamoto zinazowakabili kwani shule hiyo ilikuwa na changamoto ya ukosefu wa umeme, maji na uhaba wa walimu lakini bado amefaulu vizuri mtihani wa Taifa.
Kwa upande wake, Amour wa Sekondari ya Feza Boys ya jijini Dar es Salaam anasema alijua atafanya vizuri lakini hakujua kama atang’ara kitaifa.
“Nimepata wastani wa daraja la kwanza 1.5, sikutarajia kuwa 10 bora na nilichagua masomo haya tangu mdogo, nilipenda biashara na hesabu. Nataka nisomee uchumi,” anasema
Amour anasema saikolojia ni muhimu kwa wanafunzi kama somo wanalosoma ni gumu kwa kuwa wanatakiwa kujitahidi kurudia mara kwa mara ili kufanikisha malengo yao.
Anasema ushirikiano wa karibu kati ya walimu, wafanyakazi, wanafunzi na wazazi uliokuwepo ulisaidia kutoa motisha kwao.
Makamu mkuu wa Sekondari ya Canossa, Angelo Mlipano anasema wanafunzi 132 wamehitimu kidato cha sita mwaka huu.
Anasema matokeo hayo mazuri yametokana na juhudi binafsi za wanafunzi.
“Siku zote elimu ni kama pembe tatu baina ya mwalimu, mzazi na mwanafunzi. Walimu wetu wana moyo wa kujitolea, wapo tayari kwa hali na mali tunawapongeza. Wazazi waliiamini shule na kuwaleta watoto, ushirikiano mkubwa kati yetu wote umefanikisha,” anasema.
Kwa upande wake, mkuu wa Sekondari Feza Boys, Saimon Albert anasema mwaka jana shule hiyo ilishika nafasi ya tisa kitaifa, lakini mwaka huu vijana wamefanya kazi kubwa na kufanikiwa kushika nafasi ya tano.
“Kwanza vijana wetu ni washindani wanashindana sana inapotokea benchi imeshika nafasi fulani, wao wanajitahidi kuipita na ikitokea imefanya vizuri wanajitahidi kuishikilia nafasi ile ya juu,” anasema
Albert anasema pamoja na hayo , lakini matokeo yao yanajengwa kwa pamoja na wazazi na ni lazima wahakikishe wanawasaidia watoto kwa ushirikiano na walimu na uongozi wa shule.
“Tunachokifanya ni kujitoa kwa walimu kwa kuwatimizia (wanafunzi) wanachokihitaji katika kujiendeleza.
“Darasa la kidato cha sita lilikuwa na watoto 92, lilikuwa ni la ushindani sana na kwa kweli ni wengi kwa shule yetu kunapokuwa na kundi kubwa ushindani unakuwa juu, wao walitamani washike nafasi tatu za juu lakini kwa bahati wameshika nafasi ya tano,” anasema.