Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Shahidi akwamisha kesi ya Mdee kuendelea

Video Archive
Thu, 28 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es salaam.. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais wa Tanzania, John Magufuli inayomkabili Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imeshindwa kuendelea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kutokana na shahidi kuwa na dharura.

Wakili wa Serikali, Ashura Mzava amedai leo Alhamisi Februari 28, 2018 mbele ya  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kusikilizwa lakini shahidi ametoa udhuru kutokana na msiba.

Mzava amedai kikao kilichopita mahakama ilimuonya Mfanyakazi wa Clouds, Abdu Chemba kuja mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi wa shauri hilo lakini tangu jana ameomba udhuru kwamba wana msiba.

"Niliwasiliana na Chemba mimi mwenyewe hivyo tunaomba baada ya wiki mbili shahidi huyu aje kuendelea na usikilizwaji pia tunaomba hati ya wito kwa mashahidi wengine," amedai Mzava.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba amesema sababu zilizotolewa ni za msingi na ni udhuru ambao hauepukiki hivyo shahidi afike na wengine ili kesi iishe.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 12, 2019 kwa ajili ya kusikilizwa na ametoa hati za wito kwa mashahidi wote ili wafike kutoa ushahidi wao.

Mpaka sasa mashahidi watatu wa upande wa mashitaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo Mkuu wa Kituo cha Polisi Urafiki, Mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.

Inadaiwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno dhidi ya  Rais John Magufuli kuwa,  ‘anaongea hovyo, anatakiwa afungwe breki,’ kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kusababisha uvunjifu wa amani.



Chanzo: mwananchi.co.tz