Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Saa 12 muhimu za Dk Kigwangalla

Video Archive
Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla amezungumza na Mwananchi akiwa wodini Mwaisela katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akisema hana mengi zaidi ya shukrani kwa Mungu na wote waliomsaidia.

Huku Kigwangalla akizungumza na Mwananchi saa 30 tangu apate ajali hiyo, gazeti hili pia linakuletea hatua kwa hatua ya saa 12 za kiongozi huyo tangu apate ajali Manyara na kufikishwa Dar es Salaam juzi.

“Madaktari wananihudumia vizuri nashukuru sana, namshukuru Rais John Magufuli na viongozi wengine wote akiwamo katibu mkuu wa wizara na Bunge. Zaidi nawashukuru madaktari wote kuanzia eneo la tukio hadi hapa,” alisema Dk Kigwangalla jana saa sita mchana akiwa kwenye kitanda maalumu akipelekwa kitengo cha Radiolojia kwa ajili ya vipimo.

Waziri Kigwangalla akiwa kwenye gari na watu wengine watano alipata ajali juzi wilayani Babati mkoani Manyara iliyosababisha kifo cha ofisa habari wa wizara hiyo, Hamza Temba aliyezikwa jana Masama wilayani Hai katika mkoa wa Kilimanjaro.

Akizungumza na Mwananchi baada ya Dk Kigwangalla kufanyiwa vipimo jana, daktari wa upasuaji, Ally Mwanga alisema anaendelea vyema na hali yake inazidi kuimarika.

Dk Mwanga alisema kwamba wanarudia vipimo ili kujua maendeleo ya afya yake baada ya kuanza matibabu juzi.

Alisema majibu ya vipimo yanaonyesha kumekuwa na maendeleo mazuri ya afya ya waziri huyo.

“Dk Kigwangalla alipata majeraha sehemu mbalimbali ikiwamo mkono wa kushoto na kifua lakini tumemchunguza pia kichwani na tumboni yupo sawa na imara,” alisema Dk Mwanga.

Halima Mrisho, mdogo wa Dk Kigwangalla alisema kaka yake anaendelea vyema na matibabu.

“Kaka yangu yupo mikono salama na madaktari wamejitahidi sana. Madaktari wamemfanyia tena vipimo kwa sababu alikuwa analalamika kuwa na maumivu ya kifua,” alisema Halima.

Aliwashukuru wote wanaomhudumia kaka yake.

Wamiminika kumjulia hali

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jana saa nne asubuhi akiambatana na mkewe Mary alikwenda kumjulia hali Dk Kigwangalla.

“Hospitali ya Muhimbili ndiyo kimbilio letu kwa sasa na tunawashukuru madaktari na wauguzi kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo inaliletea heshima Taifa letu kwani hata watu wa Comoro wanakuja kutibiwa Muhimbili,” alisema Majaliwa katika taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu.

Dk Kigwangalla katika taarifa hiyo amekaririwa akisema, “Ajali ilikuwa mbaya sana hivi sasa naongea hapa namshukuru Mungu, Serikali pamoja na madaktari na wauguzi kwa jitihada kubwa walizozifanya.”

Wengine waliomjulia hali ni mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba aliyesema, “Nimefarijika kumuona pacha wangu anaendelea vyema. Namshukuru Mungu na madaktari wa mikoa ya Arusha, Manyara na (Hospitali ya) Muhimbili kwa ushirikiano wao.”

Wengine ni mbunge wa Kiembesamaki-Zanzibar, Ibrahim Raza; naibu waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; naibu waziri wa Mambo ya Nje, Dk Suzan Kolimba; katibu mkuu wa Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi na mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Saa 12 hatua kwa hatua baada ya ajali

Dk Kigwangalla alipata ajali juzi saa 12 asubuhi eneo la Vilima Vitatu wilayani Babati mkoani Manyara.

Gari lilipinduka mara tatu wakati dereva akimkwepa twiga aliyekuwa akivuka eneo hilo ambalo ni mapito ya wanyama kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwenda Hifadhi ya Manyara na kurudi.

Baada ya ajali hiyo iliyotokea jirani na moja ya malango ya kuingia eneo la Chemchem ndani ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (WMA) ya Burunge, askari wa hifadhi walijitokeza kutoa msaada.

Meneja wa taasisi ya Chemchem inayowekeza eneo hilo, Charles Sylvester alisema askari waliwaokoa majeruhi na baadaye askari wa kituo kidogo cha polisi Minjingu walifika.

Alisema eneo la tukio mtu mmoja alikuwa amefariki dunia ambaye alifahamika baadaye kuwa ni ofisa habari wa wizara, Temba. Saa moja asubuhi, Dk Kigwangalla na majeruhi wengine walichukuliwa na magari ya doria na kupelekwa kituo cha afya cha Magugu umbali wa takriban kilomita 20 kutoka eneo ilipotokea ajali.

Mwenyekiti wa Burunge WMA, Ismail Ramadhani alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika kwenye kituo hicho cha afya na kumpokea Dk Kigwangalla saa 1:33 asubuhi baada ya kupigiwa simu saa 12:30 asubuhi.

“Baada ya kupigiwa simu niliwaelekeza askari wetu wa WMA na waliokuwa na gari wajitahidi kuwawahisha majeruhi kituo cha afya Magugu ili wapate huduma,” alisema.

Ramadhani alisema alikwenda kutoa taarifa polisi Magugu ili kupatiwa hati ya matibabu (PF3). Alisema Dk Kigwangalla alipokewa na madaktari kituoni hapo na baadaye ilifika timu ya madaktari kutoka mkoani.

Alisema baada ya kukamilika huduma ya kwanza saa tano asubuhi, helikopta ilifika na kumpeleka mkoani Arusha.

Helikopta hiyo ilitua katika hoteli ya Mount Meru saa sita mchana ambako viongozi kadhaa akiwamo mkuu wa mkoa wa Arusha, Gambo; katibu mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Milanzi; waziri wa Madini, Angellah Kairuki; naibu waziri wake, Stanslaus Nyongo; waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina; wakuu wa mikoa ya Kilimanjaro, Anna Mghwira na Manyara, Alexander Mnyeti walikuwapo.

Ili kuharakisha huduma ya vipimo, Dk Kigwangalla kwa kutumia usafiri wa gari alipelekwa Hospitali ya Selian jijini Arusha.

Baada ya kupata huduma, saa kumi jioni alipakiwa kwenye gari na kupelekwa uwanja mdogo wa ndege wa Arusha alikosafirishwa kwa ndege kwenda Dar es Salaam.

Rais John Magufuli alikuwa miongoni mwa waliompokea Dk Kigwangalla katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam saa kumi na mbili jioni.

Dk Kigwangalla alipelekwa Muhimbili juzi saa moja usiku ambako anaendelea kupatiwa matibabu.

Chanzo: mwananchi.co.tz