Dar es Salaam. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Lughano Kusiluka amesema soko la ajira linahitaji watu wanaojiamini, wanaoweza kujieleza na waadilifu.
Profesa Kusiluka ameyasema hayo leo Alhamisi Septemba 19, 2019 katika Jukwaa la Fikra la kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kujadili kuwezesha vijana kuwa na ujuzi na maarifa mahsusi linalorushwa moja kwa moja na MCL Digital na televisheni ya ITV.
Amesema mitalaa ya taasisi za elimu ya juu nchini inakidhi mahitaji ya soko la ajira lakini changamoto imekuwa ni idadi kubwa ya wahitimu wakati soko la ajira bado ni dogo.
"Lazima tujiulize swali, kwa umoja wetu ni kwa namna gani tutaongeza idadi ya ajira? Ni kwa namna gani tutawaandaa vijana wetu wakiwa bado vyuoni kujiandaa na soko la ajira aidha kwa kujiajiri au kuajiriwa," amesema.
Profesa Kusiluka amesema chuo cha Mzumbe kuna kambi ya mjasiriamali ambayo inatoa fursa kwa wanafunzi kutoa mawazo yao ya ujasiriamali ambayo wanakwenda kufanya baada ya kuhitimu masomo yao.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Veronica Sarungi amesema ni muhimu kumjengea mwanafunzi ari ya ushirikiano na wenzake, hiyo inaongeza ushindani hasa kwenye ujasiriamali.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Mamia wajitokeza kushiriki Jukwaa la Fikra la Mwananchi
- LIVE MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA: KUWAWEZSHA VIJANA KUWA NA MAARIFA NA UJUZI MAHUSUSI
- VIDEO: Profesa Kusiluka achambua wanaobeza wahitimu
- VIDEO: Serikali ya Tanzania yaeleza inavyowekeza kwenye elimu
"Vijana wajue kwamba ndani yao wana uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao na vizazi vijavyo. Wasiipuuze nguvu hiyo, waifanyie kazi," amesema Sarungi wakati akichangia mada kwenye Jukwaa hilo.