Musoma/Moshi. Polisi mkoani Mara nchini Tanzania limepiga marufuku watoto chini ya miaka 18 kusherehekea sikukuu ya mwaka mpya 2020 kwa kuingia katika kumbi za disko hasa nyakati za usiku.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mara, Daniel Shillah amewaambia waandishi wa habari leo Jumanne Desemba 31, 2019 kuwa kumekuwapo na tabia ya baadhi ya wakazi wa mkoa wa Mara kuwaruhusu watoto kuingia disko jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Amesema kwa mujibu wa sheria ni marufuku kwa watoto wadogo kuingia katika kumbi za starehe nyakati za usiku hivyo jeshi lake halitakubali liendelee kutokea ndani ya mkoa wa Mara hasa nyakati za sikukuu na kwamba mmiliki wa ukumbi wa disko pamoja na mzazi atakayeruhusu mtoto kuingia disko atakamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mujibu wa sheria
"Hivi inakuwaje unamruhusu mtoto mdogo kuingia katika kumbi za starehe, huu nao ni ukatili kwa watoto na kwa vile nasi tunapambana na ukatili kwa watoto hatuwezi tukaruhusu hali kama hii iendelee katika mkoa wetu na sio kwaajili ya sikukuu tu hii ni kwa muda wote" amesema Shilla.
Kuhusu disko toto, Shilla amewataka wamiliki wa kumbi zitakazopiga disko toto kuhakikisha kunakuwapo na ulinzi wa kutosha muda wote na kwamba mwisho wa disko hilo ni saa 12 jioni.
Pia, jeshi hilo limezuia uchomaji wa matairi barabarani kama ishara ya kukaribisha mwaka mpya kwa maelezo kuwa mbali na kuhatarisha amani lakini pia vitendo hivyo vinasababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara.
"Serikali inaingia gharama kubwa katika kutengeneza miundombinu sasa sisi jeshi la polisi hatuwezi kuruhusu miundombinu hiyo kuharibiwa kisa tu watu wanasherekea mwaka mpya," amesema
Amesema jeshi lake limejipanga vema katika kuhakikisha watu wanasherehekea kwa amani na utulivu huku akiwataka watu kusherehekea kwa amani na kuepuka vitendo ambavyo vinaweza kupelekea kuwepo kwa uvunjifu wa amani ikiwamo unywaji wa pombe kupandikiza na kuacha mji bila kuwapo na ulinzi wa uhakika.