Dar es Salaam. Msajili msaidizi wa vyama vya siasa nchini Tanzania, Sisty Nyahoza na mwenyekiti wa baraza la vyama vya siasa, John Shibuda leo Jumatano Desemba 18, 2019 wamekumbana na wakati mgumu wakati wakitoa salamu katika mkutano mkuu wa Chadema baada ya kauli zao kupokewa kwa hisia tofauti na wajumbe wa mkutano huo.
Minong’ono ya wajumbe wa mkutano huo ilimlazimu mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuwatuliza baada ya kuanza kupiga kelele na kuzomea.
Katika salamu zake, Nyahoza amesema ofisi yake ni mlezi wa vyama, kuvitaka kutii sheria ya vyama vya siasa na sheria za nchi.
Baada ya kauli hiyo baadhi ya wajumbe waliguna huku wengine wakipiga kelele, “tunataka bendera zetu.”
Bendera za chama hicho zilizokuwa zimewekwa barabara ya Sam Nujoma jirani na ukumbi wa Mlimani City unakofanyika mkutano huo wa kuchagua mwenyekiti na makamu mwenyekiti, ziliondolewa na polisi jana usiku kwa agizo la mkurugenzi wa manispaa ya Ubungo, Beatrice Dominic.
"Hakuna mlezi anayependa mtoto wake asimtii. Hatupendi watoto watukutu," amesema Nyahoza huku wajumbe wakipiga makofi na kuzomea.
Hali hiyo ilimfanya mkurugenzi wa itifaki, uenezi, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema kuwaeleza wajumbe hao kuwa ujumbe kuhusu bendera ataufikisha kwa Nyahoza.
Licha ya Mrema kueleza hayo, wajumbe hao waliendelea kupiga makofi na kuzomea jambo lililomfanya Nyahoza kukatisha hotuba yake na kwenda kuketi.
Shibuda ambaye ni mwenyekiti wa chama cha Ada-Tadea naye alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wajumbe hao alipoanza kuzungumzia alivyopokelewa na kupewa nafasi ya kugombea ubunge wa Maswa mwaka 2010.
“Mimi nimetoka katika mseto wa mafiga matatu, kwanza niliwahi kugombea ubunge kupitia chama hiki pili kwa sasa ni mwenyekiti wa Ada-Tadea na tatu ni mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa,” amesema Shibuda huku miguno ikisikika.
Aliendelea kueleza kuhusu mfumo wa vyama vingi akisema alishakutana Rais John Magufuli kuzungumzia mfumo wa vyama vingi.
“Siamini kama Rais John Magufuli ana mpango wa kufuta vyama vya siasa bali hapendi kuona lugha za kudhalilishana,” amesema Shibuda na wajumbe hao kuitikia, “hawezi kufuta mfumo wa vyama vingi.”
Shibuda aliwatuliza wajumbe hao akisema, “hamjui nitamalizaje.”
Mbowe alisimama na kwenda alipokuwa amesimama Shibuda kwa lengo la kuwatuliza wajumbe hao, “hata kama hamkufurahishwa na maneno yake, muwe na nidhamu. Nidhamu ni kitu muhimu.”
Kauli hiyo ilileta utulivu katika ukumbi huo na Shibuda alizungumza kwa dakika chache na kumaliza.