Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Miili ya vijana JKT waliokufa ajalini kuagwa Mbeya leo

Video Archive
Tue, 19 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mbeya. Miili ya vijana 10 wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) waliopoteza maisha katika ajali iliyotokea Juni 14, mkoani Mbeya itaagwa leo katika kikosi cha jeshi cha 844 Itende.

Ajali hiyo iliyotokea eneo la Mwasekwa ilisababisha vifo vya vijana hao, ofisa mmoja wa JWTZ, dereva na kondakta wa basi walilopanda.

Watu wengine 46 walijeruhiwa katika ajali hiyo wakielekea Itende kwenye mafunzo ya vitendo wakitokea kambi ya Igunga mkoani Tabora.

Akizungumza na waandishi wa habari kambini Itende jana, msemaji wa JWTZ, Kanali Ramadhan Dogoli alisema shughuli ya kuaga miili ya marehemu itahudhuriwa na maofisa waandamizi wa jeshi wakiwamo mkuu wa JKT, Meja Jenerali Martin Busungu; mnadhimu mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Yakubu Mohammed na katibu mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Florens Turuka.

Alisema vijana hao wanatoka mikoa tofauti na kwamba jeshi litagharimia mazishi yao.

Kanali Dogoli alisema raia wawili waliofariki dunia katika ajali hiyo miili yao itasafirisha kupelekwa mkoani Tabora.

Hali za majeruhi

Akizungumzia afya za majeruhi wa ajali hiyo, Kanali Dogoli alisema watatu walikuwa katika hali mbaya.

Hata hivyo, alisema jana asubuhi taarifa kutoka Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ilisema wawili walianza kuzungumza na mmoja bado. Wote wapo chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Alisema majeruhi wengine wako katika Hospitali ya Kikosi cha Itende, na wengine JWTZ-Mbalizi na Hospitali ya Rufaa Mbeya kulingana na hali zao na kiwango cha matibabu wanachohitaji.

Awali, kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mussa Taibu alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa basi hilo ambaye naye alifariki papo hapo pamoja na kondakta wake.

Kamanda Taibu alisema dereva huyo hakuwa na uzoefu wa barabara hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz