Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mawakili wa Seth, Rugemarila wataka upelelezi ukamilishwe

Video Archive
Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa utetezi kwenye kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara, Herbinder Seth na mwenzake James Rugemalila wameutaka upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi kwa kuwa washtakiwa hao wamekaa rumande muda mrefu.

Washtakiwa hao wanasota rumande kuanzia Juni 19, 2017 toka walipofikishwa Mahakamani kwa mara ya kwanza kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.

Wakili wa utetezi, David Chila amedai leo Alhamisi Machi 28, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, baada ya  wakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kudai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

"Tunaomba upande wa mashtaka wakamilishe upelelezi ili kesi iweze kusikilizwa kwa kuwa washtakiwa wamekaa rumande muda mrefu sasa," alidai Chila.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi  aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 11 mwaka huu itakapotajwa tena.

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya Dola 22, 198,544.60 za Marekani na  Sh309,461,300,158.27.

Related Content

 

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Pia, inadaiwa katika mashtaka ya kujipatia fedha kwamba kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph, kwa ulaghai washtakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh309, 461,300,158.27.  

Pia, washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola 22,198,544.60 za Marekani na Sh309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni Dola 22.1 milioni za Marekani na Sh309.4 bilioni wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washtakiwa hao wapo rumande kwa kuwa mashtaka hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz