Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Maswali magumu kwa Ndugai ubunge wa Lissu

Video Archive
Wed, 3 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tangu Spika wa Bunge, Job Ndugai alipotangaza kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuitaarifu kuwa Jimbo la Singida Mashariki liko wazi baada ya mbunge wake, Tundu Lissu kutohudhuria mikutano kadhaa ya bunge huku yeye akiwa hana taarifa, kumeibuka mjadala ambao unaendelea katika majukwaa mbalimbali mojawapo likiwa ni mitandao ya kijamii.

Huko watu wamegawanyika kimtazamo kuhusiana na jambo hilo, wapo baadhi wanaitazama hatua hiyo ni sahihi na kuiunga mkono, lakini pia lipo kundi jingine linalokataa na kupingana na uamuzi huo wa spika huku wakiibua hoja mbalimbali.

Moja ya hoja za wanaopinga uamuzi wa Spika Ndugai ambao aliutoa siku ya kuahirisha Bunge la Bajeti Juni 28, mwaka huu jijini Dodoma, ni pamoja na kuwapo kwa maswali kadhaa ambayo hayajapatiwa majibu kuhusiana na suala la kutangazwa kuwa wazi kwa kiti hicho. Endapo maswali haya yatapatiwa majibu huenda ikapunguza shaka yao dhidi ya uamuzi huo.

Makamu wa Rais kumjulia hali Lissu

Novemba 29, 2017 Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alimtembelea mbunge Lissu akiwa hospitalini jijini Nairobi alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na kunusurika kuuawa.

Lissu alihamishiwa Nairobi kwa matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma alikopelekwa Septemba 7, 2017 baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika jaribio la mauaji, alipokuwa akiingia nyumbani kwake area D, Dodoma.

Pia Soma

Makamu wa Rais alimtembelea Lissu akiongozana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Pindi Chana ikiwa ni moja ya shughuli rasmi alizozitekeleza wakati alipokwenda Nairobi kushuhudia kuapishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta aliyeshinda uchaguzi mkuu wa nchi hiyo uliofanyika mwaka huo.

Wanaokosoa uamuzi wa kutangaza kuwa wazi kiti cha ubunge alichokuwa akikishilia Lissu, wanahoji kama Makamu wa Rais ambaye ni kiongozi namba mbili kwa ukubwa wa madaraka ya nchi baada ya Rais John Magufuli ametambua na kwenda hospitalini, iweje mhimili wa bunge ushindwe kufahamu hali anayopitia mbunge huyo kutafuta uimara wa afya yake.

Kauli ya waziri Ummy

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Februari mwaka huu akiwa jijini Tanga alizungumza na waandishi wa habari na kusema Serikali ipo tayari kugharamia matibabu ya Lissu na kutaka taratibu zitimizwe ili hatua hiyo itekelezwe.

Ummy alisema huku akijipambanua kuwa ndiye mwenye dhamana ya afya kuwa: “Tunaona michango hatuelewi inatoka wapi, inaweza kutumika kwa utapeli. Watanzania wanatakiwa kutuelewa kuwa tupo tayari kugharamia matibabu ya Lissu popote”.

“Mimi mwenyewe nimeumizwa na tukio la Lissu, tunaitana kama kaka na dada kwa kuwa ni mwanasheria mwenzangu. Tunaendelea kumpa pole, familia kama ipo tayari nasi tupo tayari kumtibu,” alisema Ummy.

Kwa kauli hii ya Waziri mwenye dhamana ya afya ni dhahiri Serikali ilikuwa ikifahamu kuwa Lissu ni mgonjwa na anapatiwa matibabu. Je, kama Serikali inafahamu kwa kiasi hicho na kueleza bayana kupitia waziri bado kuna haja ya kuwa na shaka na kuugua au kujiuguza kwa Lissu?

Waziri Mkuu atoa pole

Katika hotuba yake ya kuahirisha mkutano wa 11 wa Bunge la bajeti Juni 29, 2018 jijini Dodoma Waziri Mkuu ambaye ni kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni alitoa pole na kuwatakia afya njema wabunge ambao kwa wakati huo wahakuwapo bungeni kutokana na udhuru wa maradhi, Lissu alimtaja akiwa mmoja wao.

“Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu pia nitoe salamu zangu za pole na kuwatakia afya njema na uponyaji wa haraka waheshimiwa wabunge wenzetu wote ambao hawapo nasi hapa Dodoma kutokana na sababu mbalimbali za kiafya. Tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na kuendelea kulitumikia Taifa letu pamoja na wapiga kura wao. Wabunge hao ni Mheshimiwa Haji Ameir Haji (Mbunge wa Makunduchi); Mheshimiwa Nimrod Elirehemah Mkono (Mbunge wa Butiama); Mheshimiwa Tundu Antiphas Mughwai Lissu (Mbunge wa Singida Mashariki); Mheshimiwa Stephen Hillary Ngonyani (Mbunge wa Korogwe Vijijini sasa ni marehemu); na Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo (Viti Maalum),” ilisema sehemu ya hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa.

Ubunge wa Lissu ulikoma lini?

Tangu Lissu aliposhambuliwa na kulazimika kutohudhuria vikao vya Bunge, ameshakosa mikutano saba ya bunge ambayo kwa tafsri ya kauli ya Spika Ndugai ya kutokuwa na taarifa za mbunge huyo maana yake amepoteza uhalali wa kuendelea kuwa mwakilishi wa wananchi katika jimbo la Singida Mashariki.

Hata hivyo, kwa sheria na taratibu za Bunge mbunge anapoteza sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hiyo iwapo atakosa kuhudhuria mikutano mitatu ya bunge bila taarifa. Je, ni kwa nini kwa Lissu aliachwa mpaka kufikia mikutano saba akiendelea kupewa posho na stahili nyingine za kibunge.

Katika taarifa yake kuhusu michango ya wabunge Septemba 22, 2017 Bunge lilisema michango iliyochangwa inayofikia Sh43 milioni kwa ajili ya kumsaidia Lissu katika matibabu ilingizwa katika akaunti ya hospitali ya Nairobi tangu Septemba 20, 2017 hiyo ikimaanisha kuwa bunge lilitambua kilichotokea na kuguswa na matibabu yake.

Maswali haya ni baadhi ya yale yanayohojiwa ili kupata uelewa wa uhalali wa kutangazwa kuwa wazi kwa kiti hicho cha ubunge.

Chanzo: mwananchi.co.tz