Morogoro. Imelda Mlanzi, rafiki wa Jasmine Ngole aliyejiua kwa kujipiga risasi kooni na kufumua sehemu ya utosi, ameshindwa kufanya mtihani wa mwezi leo Ijumaa Februari 22, 2019.
Imelda anayesoma Shule ya Sekondari Lupanga aliachiwa shajara (diary) na marehemu Jasmin saa chache kabla ya kifo chake, leo alikwenda shule kufanya mtihani lakini alishindwa baada ya kuishiwa nguvu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
“Ni mtoto asiyewajua wazazi wake na asiyejua kazaliwa wapi? Mtoto huyu anatamani kukiona kifo chake wakati wowote, mtu yeyote atakayesoma dayari hii ndiye atakayeandika siku ya kifo chake.”
Huo ni ujumbe uliokuwa katika shajara aliouacha Jasmin aliyejiua kwa kujipiga risasi kooni na kufumua sehemu ya utosi.
Kifo chake kimeacha maswali mengi kutokana maisha aliyoishi binti huyo mwenye umri wa miaka 18 pamoja na ujumbe alioandika kwenye shajara yake na kumkabidhi Imelda waliyekuwa wakisoma naye darasa moja, siku moja kabla ya kujiua.
Mwili wa Jasmin ulikutwa kando ya barabara nyembamba, eneo la Kola B Manispaa ya Morogoro, alfajiri ya Februari 19, 2019 huku bastola aliyotumia kujiua, mali ya Profesa Hamis Maige iliyokuwa na magazine moja na ganda la risasi vikiwa kando yake.
Akizungumza na Mwananchi leo, makamu mkuu wa shule hiyo, Daud Masunga amesema kuwa Imelda alifika shuleni hapo akiwa amechelewa na baadaye hali yake ilibadilika.
Amesema alikuwa mnyonge na alikuwa akilia wakati wote hali iliyosababisha walimu wamruhusu kurudi nyumbani.
“Kwa kweli Imelda bado hayuko sawa, tumejaribu kumpa ushauri nasaha lakini bado yuko kwenye taharuki ameshindwa kufanya mitihani ya mwezi na tumemruhusu arudi nyumbani,” alisema Masunga.
Soma zaidi: VIDEO: Mwanafunzi wa kidato cha nne ajiua kwa risasi