Dar es Salaam. Maombi yaliyowasilishwa na wakili Jebra Kambole anayewatetea msanii Maua Sama na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu yatasikilizwa Septemba 26, 2018.
Kambole aliwasilisha maombi hayo dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Simon Sirro na mkurugenzi wa makosa ya Jinai Kanda Maalum (ZCO).
Katika maombi hayo yaliyowasilishwa Septemba 21, 2018, Kambole ameomba watu saba wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi kwa zaidi ya wiki moja, kupelekwa mahakamani na kusomewa mashtaka yanayowakabili sambamba na kupewa dhamana.
Maombi hayo yalifikishwa leo Septemba 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huduma Shaidi ambapo wakili Kambole aliomba watu hao saba wafikishwe mahakamani ili wasomewe mashtaka yanayowakabili na wapatiwe dhamana.
Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea watu hao walikuwa hawajafikishwa mahakamani.
Mbali na Mausa Sama, wengine ni watangazaji Shafii Dauda na Sudi Kadio maarufu Soudy Brown, Michael Mlingwa, Fadhili Kondo (meneja wa Maua), mshehereshaji Antony Luvanda na Benedict Kadege.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na wakili wa serikali, Tumain Kweka ambaye aliomba kupewa siku tatu ili waweze kuwasilisha majibu ya hati kinzani kwa maandishi.
Pia aliongeza kuwa waleta maombi waliyaleta maombi hayo na kuwapatia.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Shaidi aliamuru upande wa mashtaka kuwasilisha majibu kinzani kwa maandishi Septemba 25 na kwamba maombi hayo yatasikilizwa rasmi Septemba 26 na kuagiza siku hiyo washtakiwa waletwe mahakamani.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye waleta maombi hao waliletwa mahakamani hapo na kuhifadhiwa mahabusu.