Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mambo matano yaliyoibua mjadala Rais Magufuli akikutana na wafanyabiashara

Video Archive
Fri, 7 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli leo Ijumaa Juni 7, 2019 amezungumza na wafanyabiashara kutoka Wilaya zote nchini kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzitatua.

Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu, Dar es Salaam hoja mbalimbali zilibuka, huku baadhi zikianikwa na Rais Magufuli wakati anafungua mkutano huo ikiwamo changamoto zinazoihusu Serikali katika kushughulikia masuala ya wafanyabiashara.

Miongoni mwa mambo yaliyoibua mjadala katika mkutano huo ni pamoja na utitiri wa ushuru na kodi na Rais Magufuli kusema mpaka sasa Serikali imeshafuta tozo 101 katika sekta ya kilimo, uvuvi, ufugaji na kodi za wachimbaji wadogo wa madini.

Ukwepaji kodi ni jambo la pili lililojitokeza katika mkutano huo, kiongozi mkuu huyo wa nchi kusema ana orodha ya kampuni 17, 447 zilizosajiliwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na kukwepa kodi.

Amesema kampuni hizo zimekuwa zikiwasilisha vitabu vitatu vya taarifa za mapato na matumizi kwa mwaka, huku kitabu kinachopelekwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kikionesha faida ndogo ili kukwepa kodi, na kitabu kinachopelekwa  Benki kikionesha faida kubwa.

Rais Magufuli amezipa muda wa mwezi mmoja, kampuni hizo kuhakikisha zinalipa kodi husika.

Pia Soma

Jambo la tatu lililoibua mjadala ni kauli ya Rais kutamani atakapomaliza muda wake madarakani awe ametengeneza mabilionea 100 nchini Tanzania.

Kauli hiyo imeonekana kumfurahisha  mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),  Godbless Lema na kuandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter, “Kauli ya Rais kuwa anataka kuona Tanzania  ya mabilionea100 kabla ya utawala wake ni kauli ya matumaini kwa nchi. Kauli hii ina thamani kubwa kuliko ile ya matajiri kuishi kama mashetani. Nimemsikiliza Rais naona kama anasisitiza uwepo wa utawala bora wa sheria katika  ngazi zote za Serikali."

Suala la mbolea ya Minjingu, ni jambo la nne lililoibua mjadala baada ya mfanyabiashara wa kiwanda cha mbolea Minjingu, kumueleza Rais Magufuli changamoto anayoipata kuhusu kupata soko la mbolea kutoka katika kiwanda chake.

Rais John magufuli alimweleza mfanyabiashara huyo kuwa kuna wakati wizara ya kilimo (wakati wa Waziri Charles Tizeba), walikuwa wanaagiza mbolea kutoka nje, "Nikauliza kwanini msinunue mbolea ya Minjingu? niliambiwa wewe umekataa kuuza hiyo mbolea hadi upewe ‘capital’ fedha za serikali, ni kweli?"

Mfanyabiashara huyo alikanusha madai hayo na kusema ni maneno ya kutengenezwa.

Ufungaji wa biashara na viwanda nchini kwa kushindwa kulipa kodi ni miongoni mwa mambo yaliyoonekana kutawala katika mkutano huo.

Wafanyabiashara walieleza kero zao kuhusu namna maofisa wa TRA wanavyowasumbua na kuwafungia biashara zao kutokana na madai ya kodi.

Mfanyabiashara kutoka Singida, alimueleza Rais Magufuli kuwa wamiliki wa viwanda wanakerwa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania wanaokwenda kwenye viwanda na kuvipiga faini au kuvifunga kwa nia ya kupata sifa badala ya kuwasaidia.

Wafanyabiashara wa Tanzania wamependekeza kupunguzwa ama kuunganishwa kwa taasisi ya Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), Shirika la Viwango nchini (TBS) na TRA ili kupunguza urasimu katika upatikanaji wa vibali vya biashara na uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi ya Tanzania.

Chanzo: mwananchi.co.tz