Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Magufuli avipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kukamata dhahabu, fedha

Video Archive
Wed, 24 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais  wa Tanzania, John Magufuli amekosoa utendaji wa majeshi ya ulinzi na usalama nchini, kuhoji sababu za kilo 35 za dhahabu kutoroshwa mkoani Mwanza na kukamatwa Kenya.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 24, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kupokea madini hayo na fedha vilivyoletwa nchini na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Monica Juma aliyeambatana na mawaziri na maofisa waliotumwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Dhahabu hizo ni kilo 35.34 pamoja na fedha, vilitoroshwa mwaka 2004 kutoka Tanzania kwenda Kenya.

Magufuli na Kenyatta walikutana wilayani Chato Mkoa wa Geita hivi karibuni na kati ya mambo waliyoyajadili ni dhahabu na fedha hizo.

“Dhahabu  imetoroshwa kutoka uwanja wa ndege wa Mwanza, ikapandishwa. Mali ikaenda mpaka KIA (Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro) akaenda mpaka Kenya. Wa kupongezwa hapa kwenye hii mali ni vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya.”

“Najua wakuu wa vyombo mpo hapa, lazima niwatandike hapa hapa. Kwa sababu vimetoka uwanja wa Mwanza, vikaenda KIA, vilipofika Kenya, vile vyombo kabla ile mali haijasafirishwa kwenda Dubai vikashindwa,” amesema Magufuli.

Habari zinazohusiana na hii

Ameongeza, “Sasa unaweza ukajiuza maswali mengi, Je, ilipokuwa ikibebwa toka Mwanza vyombo vya Tanzania vilikuwa vinafanya nini?  Je vilishirikiana na mhalifu au vilimwachia? Je, dhahabu ngapi zinapita bila watuhumiwa kushikwa? Hii nawaachia ninyi.”

Hata hivyo, amesema vinafanya kazi nzuri na kwamba kuna sehemu vinalegalega.

 “Kwamba tunaachia mali mpaka inakwenda kushikwa kule. Nitaviandikia barua kupongeza vyombo vya Kenya kwa kufanya kazi nzuri. Vyombo vya ulinzi vya Kenya oyee,” amesema Magufuli.

Akizungumzia chanzo cha kurejeshwa kwa fedha hizo, Rais Magufuli amesema alimwomba Rais Kenyatta kurejeshwa kwa dhahabu hizo walipokuwa wilayani Chato.

“Hivi vitu vya fedha na dhahabu vinahitaji moyo wa jiwe na mimi nataka niwaleze, Kenyatta ni mwaminifu  ana upendo wa pekee pamoja na Serikali yake,” amesema Magufuli.

Chanzo: mwananchi.co.tz