Dar es Salaam. Siku sita za sakata la makontena 20 yanayotakiwa kupigwa mnada katika Bandari ya Dar es Salaam, zimehitishwa kwa kishindo cha aina yake.
Rais John Magufuli ameshusha nyundo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda huku akisema ni mtu mmoja tu nchini mwenye mamlaka ya kusamehe kodi na si vinginevyo.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita katika ukumbi wa wilaya hiyo akiwataka viongozi kujenga mazingira ya kuwatumikia wananchi bila kujali nafasi zao.
Kauli hiyo ya Magufuli ni kama imehitimisha mvutano kati ya Makonda mwenye makontena hayo na Waziri wa Fedha na Mipango, Philip Mpango.
Mvutano huo ulianza Jumamosi iliyopita wakati TRA ilipotaka kuyauza makontena hayo kwa mnada, lakini yakakosa wanunuzi baada ya kushindwa kufikia bei iliyotangazwa ambayo inadaiwa kuwa ni Sh60 milioni kwa kila kontena.
Kutouzika kwa makontena hayo kulimuibua Makonda, ambaye Jumapili alitoa onyo kwa mtu atakayeyanunua kuwa angemlaani pamoja na uzao wake.
Soma zaidi: RC Makonda atoa onyo kali kwa mnunuzi wa makontena yake 20
Kauli hiyo ilimfanya Waziri Mpango atembelee bandarini Jumatatu kuyakagua makontena hayo na akawataka watu kutoogopa kuyanunua.
Waziri Mpango akizungumzia makontena hayo yanayoelezwa kuwa na samani za ndani kama viti, meza na mbao za kuandikia zinazodaiwa kodi inayoelezwa kufikia Sh1.2 bilioni alisema, “Niwaombe viongozi wenzangu serikalini tuchuje maneno. Nawaomba Watanzania, anayetaka kuja kununua samani hizi asiogope, aje kununua.”
Mvutano wa viongozi hao, uliibua mjadala katika jamii na hasa mitandao ya kijamii kabla ya jana Rais Magufuli kujitokeza hadharani na kutoa msimamo wake.
Soma zaidi: Dk Mpango aagiza makontena ya Makonda yapigwe mnada
Rais Magufuli akizungumza na madiwani, viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita katika ukumbi wa wilaya hiyo aliwataka viongozi kujenga mazingira ya kuwatumikia wananchi bila kujali nafasi zao.
“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi?”
Bila ya kumtaja jina, Rais Magufuli alisema sheria za nchi zinasema wazi ni mtu mmoja tu katika nchi mwenye dhamana ya kutolipa kodi kwa mujibu wa sheria ya fedha, sheria ya madeni, sheria ya dhamana na ya misaada.
Aliitaja sheria hiyo namba 30 ya 1974, kifungu cha 3, 6, 13 na cha 15 ndicho kinampa mtu huyo dhamana ya kupokea misaada huku akisisitiza, “Hakuna mtu mwingine.”
“Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine, labda na wafanyabiashara, unasema ni makontena yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, maana yake nini?”
“Maana yake si unataka utumie walimu, ulete haya makontena, utapeleka shule mbili au tatu, ndizo zitapewa mengine unakwenda kuyauza unapeleka kwenye ‘shopping mall’ (maduka makubwa). Lakini walimu walikuambia wanahitaji makochi, sofa,” alihoji.
Rais Magufuli aliwataka wafanyakazi wasitumike kwa maslahi ya watu fulani.
Jana asubuhi, Makonda alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kinga tiba ya magonjwa ya minyoo na kichocho kwa watoto wenye umri kati ya miaka 5-14 uliofanywa Ukumbi wa Arnaoutoglou, Mnazi Mmoja, lakini aligoma kuzungumzia makontena hayo.
Mara baada ya kumaliza kufanya mahojiano na waandishi wa habari mbalimbali kuhusu kinga hiyo, Mwananchi lilimuuliza, “Mheshimiwa, unazungumziaje kuhusu makontena yako kukwama na majibu ya waziri (Mpango).”
Baada ya kuulizwa swali hilo, Makonda hakutaka kujibu chochote na kuondoka akiwaacha waandishi wa habari wakiwa wameduwaa.
Kabla ya kuanza kwa mahojiano, wasaidizi wake wa masuala ya habari walitoa tangazo, ‘Tunawaomba msiulize maswali nje ya kilichotokea,’ na baada ya Mwananchi kumuuliza swali hilo yule aliyetoa tangazo alizuia swali hilo lisipate majibu.
Mei mwaka huu, tangazo la Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA) lilichapishwa kwenye gazeti la serikali la Daily News likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia. Orodha ya wamiliki hao, ilionyesha jina la mtu aitwaye Paul Makonda aliyekuwa na makontena 20.
Kadhalika tangazo hilo lilitishia kuzipiga mnada mali hizo iwapo wamiliki hawatajitokeza ndani ya siku 30 kwa sababu tayari yalikuwa yamekaa siku 90.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda aliyakana makontena hayo na kusema si ya kwake.
“Sidhani kama nahusika na jambo lolote lile na sijui chochote, hilo unalolisema hata mimi nimesoma kwenye magazeti kama ulivyosoma wewe nafikiri zilikuwa ni habari za jana na leo nimesoma nyingine,” alisema Makonda kipindi hicho.
Baadaye, Mei 20 ilisambaa barua ya TRA, ikieleza kuwepo kwa ombi la msamaha wa kodi wa mali hizo kutoka kwa Makonda kwenda kwa Waziri wa Fedha, Philip Mpango.
Kadhalika, barua nyingine ambayo si Mamlaka ya Mapato (TRA) wala Waziri Mpango waliothibitisha kuitambua, iliandikwa na TRA kumueleza waziri husika kuwa ombi hilo haliwezekani kwa kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa haina sifa ya kupata msamaha kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya kupitia maombi hayo, tunapenda kukufahamisha kuwa sheria ya forodha ya Jumuia ya Afrika Mashariki ya 2004 na sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT) ya mwaka 2014 hazijatoa msamaha wa kulipa ushuru wa forodha na VAT kwa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa,” inaeleza barua hiyo.
Barua hiyo imetaja kiwango cha kodi hiyo kuwa ni Sh1.2bilioni ikirejea ombi la msamaha wa kodi lililowasilishwa na ofisi hiyo ya mkoa.
Kabla ya figisu hizo za msamaha wa kodi na tangazo la Serikali, Februari mwaka huu, RC Makonda aliwapeleka baadhi ya walimu wa jijini Dar es Salaam, waandishi wa habari na wadau wengine kwenda bandarini ambako aliwaonyesha makontena yenye vifaa vya ofisi na vya kufundishia, akisema vimetolewa na Watanzania waishio Marekani.
Jumamosi iliyopita, TRA ilifanya mnada wa kwanza wa kuuza makontena hayo ambayo hata hivyo yalikosa wanunuzi.
Alipopigiwa simu siku hiyo kuhusu mnada huo, Makonda alisema:
“Sina taarifa ya kupigwa mnada wa hivyo vifaa, mimi nipo msibani Mwanza, ila kauli yangu kwa walimu ambao ninawajali na kuwapenda, wasikate tamaa, nawapenda sana, ujumbe wangu mkubwa kwao ni wamtegemeao Mungu ni kama Mlima Sayuni hawatatikisika kamwe.”
Lakini siku iliyofuata Jumapili ya Agosti 26, Makonda baada ya kusali katika Kanisa la Anglikana mjini Ngara mkoani Kagera alizungumzia suala hilo la makontena yake kupigwa mnada akisema atahakikisha hayauzwi na badala yake yanapelekwa kwa walimu kama alivyokusudia.
“Leo (Jumapili) nimekwenda katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Anglikana mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwani naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa mkoa wangu,” alisema Makonda.
“Nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwani vya madhabahuni havichezewi,”alisema Makonda.
Hata hivyo, Jumatatu Agosti 27, Mpango alifanya ziara ya kushtukiza bandari kavu ya Dar es Salaam (DICD) na akatumia fursa hiyo kutoa onyo kwa watendaji wa serikali.
Dk Mpango alisema wanachokifanya ni kusimamia sheria za nchi ambazo hazichagui sura wala cheo cha mtu.
“Niliapa kutekeleza sheria za nchi na sheria za kodi. Katika usimamizi wa sheria hizi, kamishna zisimamie bila kuyumba. Piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu. Sheria inasema mzigo ulioagizwa kutoka nje hauna msamaha wa kodi. Hivyo, mchakato ulioanza kuutekeleza endeleeni nao,” alisema Dk Mpango akimuelekeza kamishna wa Forodha, Ben Usaji.
Dk Mpango alisema; “Niwaombe viongozi wenzangu serikalini tuchuje maneno. Nawaomba Watanzania, anayetaka kuja kununua samani hizi asiogope, aje kununua. Haipendezi kusikia eti mtu atakayenunua samani hizi atapata laana, tena ya Mungu. Kwa nini tunahusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii? Nawaomba Watanzania anayetaka kuja kununua samani hizi aje, hakuna cha laana wala nini.”
“Kamishna piga mnada mara ya kwanza, ya pili, ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu. Hata mimi ningekuwa na hela ningekuja kununua tuone hiyo laana inatoka wapi,” alisema Waziri Mpango.
Soma zaidi: Makonda ayakana makontena ya Paul Makonda bandarini