Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad leo Jumatatu Machi 18, 2019 ametangaza yeye, viongozi, pamoja na wafuasi wanaomuunga mkono kuhamia Chama cha ACT- Wazalendo.
Maalim Seif ametangaza uamuzi huo zikiwa zimepita saa chache tangu Mahakama Kuu ya Tanzania kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba ndani ya CUF hali iliyomweka kando Maalim Seif.
Akizungumza na waandishi wa habari mchana wa leo Jumatatu katika ofisi za wabunge wa CUF Magomeni jijini Dar es Salaam, Maalim Seif amesema mapambano ya kisiasa lazima yaendelee.
“Mimi na wenzangu, tumetafakari kwa kina juu ya uamuzi wa kesi ulivyokwenda, tumeona kutafuta jukwaa jingine la kulitumia kuwa ni ACT- Wazalendo,” amesema Maalim Seif.
“Nawatangazia Watanzania wote na wanachama wote waliokuwa wanatuunga mkono mimi na wenzangu, tunajiunga na ACT- Wazalendo, tunawaomba wote wajiunge ili kuendeleza kazi kubwa tuliyokuwa tumeianza,” amesema.
Maalim Seif amewashukuru wale wote waliojitolea nyumba zao kwa ajili ya ofisi za CUF na kuomba waendelee kufanya hivyo wakiwa ACT- Wazalendo.
“Mapambano ya kujenga demokrasia sio kazi ya lele mama, tumefanya kazi kubwa hadi hapa tulipofikia,” amesema .
Amesema tukio hili ni historia mpya kote Zanzibar na Bara, “umma haujawahi kushindwa kokote duniani, ndiyo historia inaonyesha, hatuna wasiwasi kuwa umma wa Watanzania nao utashinda.”
Kuhusu kuhama na nyadhifa zake, Maalim Seif amesema wanahamia huko pasina masharti wala vyeo na wanakwenda kama wanachama wa kawaida na ikiwa watapewa vyeo watavichukua au la.
Akizungumzia nafasi ya wabunge amesema ni wana CUF, wengi wanawaunga mkono wao, “Tumewaachia wenyewe, kama watahama sasa au baadaye ni wenyewe, uamuzi wataamua wenyewe.”
Soma zaidi: Samani za ofisi CUF Zanzibar zaanza kuhamishwa